Yanga yaifuata JKT Tanzania nusu fainali, ikiichakaza Stand United

Muktasari:
- Staa wa mchezo huo uliochezwa Jumanne hii alikuwa kiungo wa Yanga, Stephane Aziz KI aliyepiga mabao manne huku Clatous Chama akifunga mawili. Beki Nickson Kibabage na mshambuliaji Kennedy Musonda wakifunga moja kila mmoja.
YANGA ilichowafanyia Stand United ni kitu cha kikatili sana, baada ya kuichakaza kwa mabao 8-1, kwenye mchezo ambao iliutawala vyema, ikiwafuata JKT Tanzania katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).
Staa wa mchezo huo uliochezwa Jumanne hii alikuwa kiungo wa Yanga, Stephane Aziz KI aliyepiga mabao manne huku Clatous Chama akifunga mawili. Beki Nickson Kibabage na mshambuliaji Kennedy Musonda wakifunga moja kila mmoja.
Yanga ilizimaliza dakika 45 za kwanza wakiwa juu wakiongoza kwa mabao 4-0 wakiutawala vizuri mchezo huo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar kwa mabao ya Aziz KI dakika ya 16, Kibabage (dk 20) na mawili ya Chama dakika za 32 na 41, huku Stand wakitoka bila kupiga shuti hata moja lililolenga lango.
Kipindi cha pili, Stand walirudi kwa nguvu na kufanikiwa kupata bao dakika ya 48 kupitia Msenda Senda akiwazidi akili mabeki wa Yanga na kufunga bao kali.
Bao hilo likawa kama limewakera Yanga na kuwa mwiba mkali, Aziz KI akafunga mabao matatu kwenye dakika za 51, 60 na 64
Mshambuliaji Kennedy Musonda aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Aziz KI akamalizia karamu hiyo ya mabao akipiga bao la nane dakika ya 86 lililomaliza mchezo huo.
Matokeo hayo sasa yanaifanya Yanga kuifuata JKT Tanzania ambayo ilitangulia kukata tiketi ya kucheza nusu fainali baada ya kuichapa Pamba Jiji mabao 3-1.
NUSU FAINALI ITAKAVYOKUWA
Hatua ya nusu fainali mechi zitachezwa Mei 16 na 17 mwaka huu kwenye viwanja ambavyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) itapanga.
Katika hatua hiyo ya nusu fainali itazikutanisha timu zote za Ligi Kuu Bara, Yanga itacheza dhidi ya JKT Tanzania huku Simba ikipambana na Singida Black Stars.
JKT Tanzania imefuzu nusu fainali baada ya kuifunga Pamba Jiji mabao 3-1 katika mchezo wa robo fainali uliochezwa Jumatatu hii kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar.
Singida Black Stars nayo ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida, iliifunga Kagera Sugar mabao 2-0 hatua ya robo fainali.
Simba ilikuwa ya kwanza kufuzu nusu fainali, baada ya Jumapili iliyopita kuifunga Mbeya City mabao 3-1, kisha Yanga ikafunga hesabu ya timu nne kufuatia kuichapa Stand United mabao 8-1. Yanga inapambana kuhakikisha inatetea ubingwa wa michuano hiyo ilioubeba mara tatu mfululizo.