Ndayiragije aipa ubingwa Kenya Police ikizima utawala wa Gor Mahia

Muktasari:
- Timu hiyo yenye maskani yake Nairobi, imetwaa ubingwa huo baada ya kuichapa Shabana FC bao 1-0 katika mechi ya raundi ya 33 iliyochezwa leo Juni 15, 2025 kwenye Uwanja wa Kenyatta uliopo Machakos.
KOCHA wa zamani wa Azam, KMC na Timu ya Taifa ya Tanzania, Etienne Ndayiragije, ukiwa ni msimu wake wa kwanza ameiongoza Kenya Police FC kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya 2024/2025 kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo tangu ilipopanda daraja mwaka 2021.
Timu hiyo yenye maskani yake Nairobi, imetwaa ubingwa huo baada ya kuichapa Shabana FC bao 1-0 katika mechi ya raundi ya 33 iliyochezwa leo Juni 15, 2025 kwenye Uwanja wa Kenyatta uliopo Machakos.
Bao la Brain Okoth dakika ya 75 kwa kichwa akiunganisha mpira wa pigo la kona, lilitosha kuipa ushindi Kenya Police na kutwaa ubingwa ikisalia raundi moja kuhitimisha msimu huu wa ligi hiyo.
Kenya Police imeivua ubingwa Gor Mahia ambayo licha ya kushinda 3-2 dhidi ya Ulinzi Stars, lakini tofauti ya pointi na michezo iliyobaki haiwezi kubadili chochote hata ikishinda mechi ya mwisho.
Gor Mahia ilikuwa bingwa mtetezi wa ligi hiyo ikitwaa ubingwa kwa misimu miwili mfululizo 2022-2023 na 2023-2024, huku ikiwa ndio bingwa wa kihistoria ikitwaa mara nyingi ambazo ni 21.
Polisi Kenya imefikisha alama 64 ikiongoza msimamo wa ligi ikibakiza mechi moja wikendi ijayo dhidi ya Gor Mahia iliyo nafasi ya pili na alama 58. Kwa sasa timu zote 18 zinazoshiriki ligi hiyo zimecheza mechi 33 kila moja.
Mchezo wa mwisho Jumapili ijayo, Gor Mahia italazimika kuwapigia makofi mabingwa wapya, Kenya Police wakati wa kuingia uwanjani ikiwa ni heshima kwa wawakilishi hao wa Kenya katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Katika mechi nyingine, Kakamega Homeboyz imepanda hadi nafasi ya tatu baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bidco United katika mchezo uliochezwa pia leo jioni kwenye Uwanja wa Thika.
MATOKEO YA MECHI ZINGINE:
Mara Sugar 0-0 Murang’a Seal
FC Talanta 1-3 AFC Leopards
Mathare United 0-0 Bandari FC
Tusker 0-0 Kariobangi Sharks