Pamba Jiji, Azam FC vita ya nne Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Pamba Jiji ipo nafasi ya nne katika msimamo ikikusanya pointi 23 kupitia mechi 14 ilizocheza inatarajia uwanja wa nyumbani, CCM Kirumba, jijini Mwanza kuikaribisha Azam iliyocheza mechi 10 na kuvuna pointi 22 ikiwa ni muendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara itakayopigwa Jumatatu Machi 2, 2026.
KOCHA Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema anatarajia dakika 90 bora dhidi ya Azam FC ambazo amezitaja kuwa zitaamua hatma ya nani kubaki nafasi ya nne huku akisisitiza kuwa wamejianda kushindana na anatambua wanakutana na timu bora.
Pamba Jiji ipo nafasi ya nne katika msimamo ikikusanya pointi 23 kupitia mechi 14 ilizocheza inatarajia uwanja wa nyumbani, CCM Kirumba, jijini Mwanza kuikaribisha Azam iliyocheza mechi 10 na kuvuna pointi 22 ikiwa ni muendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara itakayopigwa Jumatatu Machi 2, 2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza alisema wanatambua wanaenda kukutana na timu bora iliyo sheheni nyota wengi wazoefu lakini hilo haliwapi hofu kwani na wao wanakikiso bora na imara wataingia katika mchezo huo kuhakikisha wanabakiza pointi tatu nyumbani.
“Azam FC ni timu nzuri ina wachezaji bora na benchi la ufundi lenye mbinu bora hilo kila mmoja analifahamu soka ni mchezo wa makosa atakayetumia vizuri nafasi ndiye atakayeibuka na matokeo kwa upande wangu nimewaandaa vizuri wachezaji wangu kimbinu na kisaikolojia natumai watafanya vizuri,” alisema kocha huyo raia wa Kenya na kuongeza;
“Tutakuwa na dakika 90 bora kwa pande zote mbili timu itakayochanga vyema karata zake ndio itakayopata matokeo ambayo ni muhimu kwa pande zote mbili kutokana na malengo ya timu zote naheshimu ubora wa mpinzani wangu sina presha yoyote.”
Baraza alisema wanatembea na malengo yao kwenye kila mchezo hivyo wataingia kwa kumheshimu mpinzani wao huku wakifanyia kazi kile wanachokihitaji ilo waendelee kujihakikishia nafasi ya kuendelea kubaki walipo.
“Haitakuwa rahisi kwani tunakutana na timu ambayo imetoka kupata matokeo kwenye mechi mbili mfululizo nyumbani na ugenini lakini hilo halitupi presha tunazongatia maandalizi zaidi na kufanya kile ambacho kitatufanya tuendelee kusalia nafasi ya nne baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza.”
Wakati huohuo, Baada ya kuambulia sare ya 1-1 ugenini katika Ligi Kuu dhidi ya Namungo, benchi la ufundi la Singida Black Stars limetamba kwamba kwa sasa limeanza hesabu mpya za kubeba pointi tatu kutoka kwa Wagosi wa Kaya, Coastal Union watakaovaana nao keshokutwa Jumatatu, mjini Singida.
Singida ilijikuta ikinyang'anywa tonge mdomoni dakika za jioni na wenyeji Namungo baada ya awali kuongoza kwa bao 1-0 la penalti ya Elvis Rupia kabla ya kinara wa mabao wa Ligi, Fabrice Ngoy kuchomoa, ila kocha wa timu hiyo ametamba wameshajua makosa na Coastal Union kazi wanayo.
Kocha David Ouma alisema katika soka kuna nyakati za kiuchezaji kulingana na mechi husika wanazozitumia kuhakikisha timu inapata matokeo ya ushindi na hili ndilo lililotokea kwenye Uwanja wa Majaliwa, uliopo Ruangwa mkoani Lindi dhidi ya Namungo.