Arsenal yafuzu nusu fainali UEFA na rekodi yake
Muktasari:
- The Gunners waliingia kwenye mchezo huo uliochezwa usiku wa Aprili 15, 2026 wakiwa na ushindi wa 1-0 kutoka mechi ya kwanza, shukrani kwa bao la dakika za mwisho la Kai Havertz walilolipata nchini Ureno wiki iliyopita, na bao hilo lilitosha kabisa kukiwezesha kikosi cha Mikel Arteta kufuzu kwenda hatua ya nne bora.
ARSENAL imefanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Sporting kwenye Uwanja wa Emirates, huku ikiendelea kushikilia rekodi yake ya kuwa timu pekee isiyopoteza katika michuano hiyo msimu huu ikishinda mechi 10 na sare mbili.
The Gunners waliingia kwenye mchezo huo uliochezwa usiku wa Aprili 15, 2026 wakiwa na ushindi wa 1-0 kutoka mechi ya kwanza, shukrani kwa bao la dakika za mwisho la Kai Havertz walilolipata nchini Ureno wiki iliyopita, na bao hilo lilitosha kabisa kukiwezesha kikosi cha Mikel Arteta kufuzu kwenda hatua ya nne bora.
Arsenal ilianza mchezo kwa kasi kubwa na kuonekana kutawala umiliki wa mpira, lakini licha ya hilo, ilikuwa ni Sporting iliyokuwa hatari zaidi katika kipindi cha kwanza.
Francisco Trincao, Pedro Goncalves pamoja na kosa la pasi kutoka kwa kipa wa Arsenal, David Raya, iliwapa Sporting nafasi kadhaa za kufunga kabla ya Geny Catamo kupiga mpira uliogonga mwamba baada ya kupokea krosi kutoka kwa Maxi Araujo ndani ya eneo la hatari.
Kadri mchezo ulivyoendelea, hali ya taharuki ilitawala kwa mashabiki wa nyumbani, huku Arsenal ikijitahidi kulinda ushindi wake mwembamba, hasa baada ya kupoteza dhidi ya Bournemouth kwenye Ligi Kuu England mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika kipindi cha pili, Araujo alipata nafasi nzuri zaidi kwa Sporting lakini alipiga mpira uliokwenda nje akiwa ndani ya eneo la hatari, huku mchezaji wa akiba Leandro Trossard akigonga mwamba kwa kichwa baada ya mpira wa kona mwishoni mwa mchezo kwa upande wa Arsenal.
Ushindi huo wa jumla, unamaanisha kuwa Arsenal wamefanikiwa kufika nusu fainali ya michuano hiyo kwa misimu miwili mfululizo kwa mara ya kwanza katika historia yao, na sasa watakutana na Atletico Madrid kuwania nafasi ya kufika fainali.
Atletico Madrid imefuzu nusu fainali baada ya Aprili 14, 2026 kuiondosha Barcelona kwa jumla ya mabao 3-2, kufuatia ugenini kushinda 2-0 na nyumbani kuchapwa 2-1.
Mechi hiyo ya nusu fainali, Atletico itaanzia nyumbani Aprili 29, 2026 ikiikaribisha Arsenal jijini Madrid, kisha marudiano kule London Mei 5, 2026.