Arsenal yapata mrithi wa Partey

Muktasari:
- Norgaard, ambaye ni raia wa Denmark mwenye umri wa miaka 31, yuko mbioni kujiunga na Arsenal, na sasa kinachosubiriwa ni kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kukamilisha uhamisho wake huo.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imefanikiwa kufikia makubaliano ya kumsajili kapteni wa Brentford, Christian Norgaard, kwa ada ya pauni 10 milioni pamoja na nyongeza ya hadi Pauni 5 milioni, ili akawe mbadala wa kiungo Thomas Partey ambaye imeshindwa kufika naye makubaliano ya kusaini mkataba mpya.
Norgaard, ambaye ni raia wa Denmark mwenye umri wa miaka 31, yuko mbioni kujiunga na Arsenal, na sasa kinachosubiriwa ni kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kukamilisha uhamisho wake huo.
Licha ya hadi sasa kuwa bado Arsenal haijafikia mwafaka kuhusu maslahi binafsi kati yao na wawakilishi wa kiungo huyo, ripoti zinaeleza dili hilo lina asilimia zaidi ya 90 za kukamilika.
Mkataba wa Partey unamalizika mwishoni mwa mwezi huu, na ingawa Arsenal haijafunga milango kuhusu uwezekano wa kuendelea naye, hatua ya haraka ya kumsajili Norgaard inaonyesha kuwa haiko tayari kulazimishwa kukubali madai makubwa ya mshahara ya mchezaji huyu.
Norgaard anatarajiwa kuimarisha safu ya kiungo ya Mikel Arteta kutokana na uzoefu wake wa Ligi Kuu England.
Alisaini mkataba mpya wa miaka miwili na Brentford Machi mwaka huu licha ya kwamba alipokea ofa kutoka kwa Benfica.
Hata hivyo, wazo la kujiunga na Arsenal ili kushinda mataji na kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya mwisho ya maisha yake ya soka ni jambo linaloonekana kumvutia.
Brentford imekuwa ikilengwa na timu kubwa nyingi ambazo zinasajili wachezaji tangu kuanza kwa dirisha hili.
Tayari imeshampoteza kocha mkuu Thomas Frank pamoja na watu watatu wa benchi lake la ufundi waliohamia Tottenham.
Pia, Manchester United iko karibu kufikia makubaliano ya kutoa pauni 60 milioni kwa ajili ya kumsajili Bryan Mbeumo, mshambuliaji wa kimataifa wa Cameroon.
Norgaard pia alikuwa chaguo la Frank, aliyewahi kumfundisha katika timu za vijana za taifa la Denmark na Brondby.