Bayern yaipiga Madrid nje ndani, yaifuata PSG
Muktasari:
- Mabao matano yalifungwa katika kipindi cha kwanza chenye kasi kubwa kwenye mchezo huo wa marudiano wa robo fainali uliochezwa usiku wa Aprili 15, 2026 pale Alianz Arena jijini Munich, Ujerumani, kabla ya mchezo kubadilika na kuwa wa mbinu zaidi kipindi cha pili huku timu zote zikishusha kasi.
BAYERN Munich imeifuata Paris Saint-Germain hatua ya nusu fainali ya UEFA Champions League baada ya kuibuka washindi katika mchezo wa kusisimua wenye mabao saba dhidi ya Real Madrid.
Mabao matano yalifungwa katika kipindi cha kwanza chenye kasi kubwa kwenye mchezo huo wa marudiano wa robo fainali uliochezwa usiku wa Aprili 15, 2026 pale Alianz Arena jijini Munich, Ujerumani, kabla ya mchezo kubadilika na kuwa wa mbinu zaidi kipindi cha pili huku timu zote zikishusha kasi.
Ilionekana kama muda wa nyongeza ungehitajika kuamua mshindi, lakini mchezaji wa akiba wa Real Madrid, Eduardo Camavinga, alionyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kupoteza muda kufuatia kumchezea vibaya Harry Kane dakika nne kabla ya muda kuisha.
Dakika moja kabla ya mwisho, Luis Díaz alitoa pigo la mwisho kwa kufunga bao lake la 24 msimu huu.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool alicheza pasi ya kugongeana (one-two) na Jamal Musiala kabla ya kupiga shuti lililoingia wavuni juu.
Real Madrid walikuwa wakiongoza mara tatu, lakini Kane alifunga bao lake la 50 msimu huu huku Bayern, waliokuwa na ushindi wa 2-1 kutoka mchezo wa kwanza, wakijibu kila walipofungwa.
Hatimaye walihakikisha hakuna muujiza kutoka kwa mabingwa hao wa Ulaya mara 15 baada ya Michael Olise kufunga bao la nne katika muda wa nyongeza, na kuifanya Bayern kushinda 4-3 usiku huo na 6-4 kwa jumla.
Sasa Bayern inakwenda kukutana na PSG hatua ya nusu fainali iliyoiondosha Liverpool kwa jumla ya mabao 4-0.
Mechi ya kwanza hatua ya nusu fainali, PSG itaikaribisha Bayern Aprili 28, 2026, kisha zitarudiana kule Ujerumani, Mei 6, 2026.