Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Carlo ampa Neymar tumaini la mwisho

NEYMAR Pict

Muktasari:

  • Kombe la Dunia 2026 linatarajiwa kufanyika Marekani, Mexico na Canada kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.

BRASILIA, BRAZIL: KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Carlo Ancelotti amempa Neymar Jr matumaini ya kurejea katika timu ya taifa baada ya kumjumuisha kwenye kikosi cha awali cha wachezaji 55 kwa ajili ya Kombe la Dunia 2026.

Kwa muda mrefu kumekuwapo na mashaka kuhusu nafasi ya Neymar kutokana na majeraha ya mara kwa mara na hali yake ya utimamu wa mwili, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa nchini humo kiasi cha wakati fulani rais Lula Da Silva wa taifa hilo kuzungumzia suala hilo hadharani akitaka hatima yake imalizwe kwa weledi.

Awali, Ancelotti alikuwa amesema wazi kuwa atawaita wachezaji walio fiti kwa asilimia 100 kwa ajili ya fainali hizo, jambo lililosababisha Neymar kukosekana katika mechi za kirafiki dhidi ya Ufaransa na Croatia zilizopigwa Marekani, Machi, mwaka huu.

Hata hivyo, Neymar ametumia muda wake wa kupona majeraha kurejea uwanjani akiwa na kikosi cha klabu yake ya Santos huku akiongeza dakika za kucheza na kurejesha makali yake ya kufunga mabao.

Mwandishi maarufu wa habari za uchunguzi na tetesi za usajili Fabrizio Romano ameripoti kuwa Neymar amejumuishwa kwenye kikosi cha awali, lakini uamuzi wa mwisho kuhusu kikosi rasmi cha wachezaji 26 utatangazwa wiki ijayo.

Nyota huyo ameifungia Santos mabao sita na kutoa pasi tatu za mabao katika mechi 13 alizoichezea msimu huu.

Neymar hajaichezea Brazil tangu Oktoba 17, 2023 alipoumia goti katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Uruguay, na licha ya kujumuishwa kwenye kikosi cha awali, nafasi yake katika kikosi cha mwisho bado haijathibitishwa.

Kombe la Dunia 2026 linatarajiwa kufanyika Marekani, Mexico na Canada kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.