Chelsea yapewa uwanja London

Muktasari:
- Chelsea wanapanga kupanua Stamford Bridge ili uweze kuchukua mashabiki 60,000 badala ya 42,000 wa sasa, lakini watahitaji uwanja wa muda wakati ukarabati ukiendelea.
LONDON, ENGLAND: MKURUGENZI wa shirikisho la mchezo wa Rugby England, Bill Sweeney, yupo tayari kuwaruhusu Chelsea kutumia Uwanja wa Twickenham wakati wanaufanyia maboresho uwanja wao wa Stamford Bridge.
Chelsea wanapanga kupanua Stamford Bridge ili uweze kuchukua mashabiki 60,000 badala ya 42,000 wa sasa, lakini watahitaji uwanja wa muda wakati ukarabati ukiendelea.
Tottenham Hotspur waliwahi kucheza Wembley kati ya 2017 na 2019 walipokuwa wanajenga uwanja wao mpya.
Inaaminika Sweeney anataka kuwakaribisha Chelsea kwa misimu miwili akiamini itawasaidia kupata mapato makubwa kwa kuwakodisha.
Sweeney anasisitiza uwanja huo una leseni ya kuandaa mechi za Ligi Kuu, lakini ana hofu halmashauri ya mtaa wa Richmond huenda ikazuia mpango huo.
Sweeney alisema:"Itakuwa na faida kubwa kifedha. Leseni inaruhusu jambo hilo kufanyika na tayari kulikuwa na mazungumzo hapo awali kuhusu timu za Ligi Kuu kucheza hapa. Halmashauri ya Richmond inajali zaidi athari zinazoweza kutokea kwa wakazi wa eneo hilo, idadi ya mashabiki na kadhalika, hivyo itategemea ni klabu gani. Najua watakuwa tayari kuzungumza kuhusu hilo."
Hivi karibuni, Sweeney alitishia kuhamisha makao ya timu ya taifa ya England kutoka Twickenham hadi Midlands na Milton Keynes kutokana na mzozo kuhusu tamasha la Beyonce ambalo lilitakiwa kufanyika katika uwanja huo.
Halmashauri ilikataa kutoa kibali kwa sababu tayari idadi ya matamasha yanayoruhusiwa kufanyika kwenye uwanja huo kwa mwaka ambayo ni matatu yalikuwa yameshatimia, hivyo hakukuwa na tamasha lingine lililoruhusiwa hadi pale mwaka utakapopinduka.