Nkuku anavyotolewa macho viunga vya Arsenal

Muktasari:
- Tangu kuanza kwa msimu huu Arsenal imekuwa ikipata tabu katika eneo la ushambuliaji hususan namba tisa ambapo kuna wakati ililazimika kumtumia Kai Havertz ambaye sio namba yake kiasili.
ARSENAL inafikiria kumsajili straika wa Chelsea na timu ya taifa ya Ufaransa, Christopher Nkunku, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa ni katika lengo la kuboresha safu ya ushambuliaji.
Tangu kuanza kwa msimu huu Arsenal imekuwa ikipata tabu katika eneo la ushambuliaji hususan namba tisa ambapo kuna wakati ililazimika kumtumia Kai Havertz ambaye sio namba yake kiasili.
Nkuku ni miongoni mwa washambuliaji ambao Chelsea ipo tayari kuwauza katika dirisha lijalo baada mwenyewe kuomba kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza.
Tangu kuanza kwa msimu amecheza mechi 42 za michuano yote na kufunga mabao 14. Mkataba wake unamalizika 2029.
Jamie Gittens
CHELSEA imepanga kumsajili winga wa Borussia Dortmund na England, Jamie Gittens, 20, kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia upande kwa klabu. Gittens, miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Dortmund tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao 12. Mkataba wake unamalizika 2028.
Tomas Soucek
KOCHA wa Everton, David Moyes, amewasilisha jina la kiungo wa West Ham United na timu ya taifa ya Jamhuri ya Czech, Tomas Soucek, 30, akitaka asajiliwe katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Soucek ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha West Ham United, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika ifikapo 2027.
Lucas Paqueta
MABOSI wa West Ham United wanahitaji kiasi kisichopungua Pauni 70 milioni ili kumuuza kiungo wa kimataifa wa Brazil, Lucas Paqueta, 27, dirisha la majira ya kiangazi ikiwa ni sehemu ya kukusanya pesa kwa ajili kwa ajili ya kuboresha kikosi. Paqueta ambaye mkataba unamalizika 2027, msimu huu amecheza mechi 33 michuano yote akifunga mabao matano.
Leroy Sane
WINGA wa Bayern Munich, Leroy Sane, 29, amekataa ofa nono inayofikia Pauni 80 milioni kutoka Saudi Arabia ili kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Bayern Munich. Sane ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, awali alikuwa akihusishwa kutua Arsenal na Liverpool ndizo zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa ya kumpata.
Dario Essug
CHELSEA inatarajiwa kukamilisha dili la kumsajili kiungo wa Sporting Lisbon na Ureno, Dario Essugo katika dirisa lijalo la majira ya kiangazi mwaka huu kwa ada inayodaiwa kufikia Pauni 21 milioni baada ya kuvutiwa na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu akiwa Las Palmas anayoichezea kwa mkopo wa msimu mmoja. Mkataba wa Dario na Lisbon unatarajiwa kumalizika 2027.
Jarrad Branthwaite
REAL Madrid bado inamtazama beki wa Everton na timu ya taifa ya England, Jarrad Branthwaite mwenye umri wa miaka 22 kama miongoni mwa wachezaji inaoweza kuwasajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi mwaka huu. Mchezaji huyo amekuwa na kiwango bora katika kikosi chake na kuna wakati alihusishwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu England ikiwamo Man United.
Idrissa Gueye
EVERTON ipo katika mazungumzo na wawakilishi wa kiungo raia wa Senegal, Idrissa Gueye, 35, kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu zaidi. Gueye ambaye ni miongoni mwa viungo tegemeo wa Everton, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Fundi huyo tangu kuanza kwa msimu amecheza mechi 36.