Dakika hatari za mabao Euro 2024

Muktasari:

  • Mfano mechi ya England na Slovenia, iliyomalizika kwa matokeo ya sare ya bila kufungana, kuna baadhi ya picha ziliwaonyesha mashabiki wakiwa wanasinzia majukwaani. Kwenye fainali hizo za Euro 2024, kwa mechi zilizochezwa kwenye hatua ya makundi, nne tu ndizo zilikosa mabao. Ni zile za Denmark na Serbia, England na Slovenia, Uholanzi na Ufaransa na Ukraine na Ubelgiji.

MUNICH, UJERUMANI: RAHA ya mechi bao. Si ndo hivyo. Ndiyo maana, hata kwenye Euro 2024, mechi zilizomalizika kwa matokeo ya kutoshuhudia bao lolote, hazikuleta mzuka mwingi kwa mashabiki wa fainali hizo zinazoendelea huko Ujerumani.

Mfano mechi ya England na Slovenia, iliyomalizika kwa matokeo ya sare ya bila kufungana, kuna baadhi ya picha ziliwaonyesha mashabiki wakiwa wanasinzia majukwaani. Kwenye fainali hizo za Euro 2024, kwa mechi zilizochezwa kwenye hatua ya makundi, nne tu ndizo zilikosa mabao. Ni zile za Denmark na Serbia, England na Slovenia, Uholanzi na Ufaransa na Ukraine na Ubelgiji.

Nyingine zote zilizobaki kwenye hatua hiyo ya makundi, makipa waliokota mipira kwenye nyavu zao na kuwapa mashabiki mzuka wa kushangilia mabao.

Mabao 81 yamefungwa kwenye hatua hiyo ya makundi na ni sawa na wastani wa mabao 2.25 kwa kila mechi, ikiwa ni wastani wa dakika 40 kwa kila bao.

Timu zilizotisha kwa kufunga mabao ni Ujerumani (mabao 8), Austria (mabao 6), Uturuki, Uswisi, Hispania na Ureno (zilizofunga mabao 5 kila moja). 

Ushajiuliza ni dakika gani hatari kwa mabao kwenye fainali hizo za Euro 2024? Kwenye fainali hizo za Ujerumani, mambo yapo hivi juu ya dakika hatari za mabao.

Kuanzia dakika 1 hadi 15, yamefungwa mabao 13, likiwamo lile la mapema zaidi lililofungwa na mkali wa Albania, Nedim Bajrami, aliyefunga kwenye sekunde ya 23.

Dakika 16-30 mashabiki wameshuhudia mabao 17 yakitinga kwenye nyavu, na kuonyesha kuwa ni dakika hatari zaidi, kutokana na kushuhudia mabao mengi katika fainali hizo, huku dakika 31-45 ikishuhudia mabao sita tu.

Kwenye dakika 45+ ni mabao matatu tu ndiyo yaliyofungwa kwenye dakika hizo katika fainali hizo za Euro 2024, huku dakika 46-60 ikishuhudia mabao 12, ambayo yanafanya kuwa dakika hatari zaidi kwa mabao katika kipindi cha pili.

Dakika 61-75 imeshuhudia mabao 11, huku dakika 76-90 yamefunga mabao tisa na zile za dakika 90+ ni habari zaidi kwenye fainali za Euro 2024 baada ya kushuhudia mabao 10 yakifungwa kwenye muda huo wa dakika za majeruhi.

Wanaoongoza kwa mabao ni Mikautadze wa Georgia, aliyefunga mara tatu, wakati Musiala wa Ujerumani, Gakpo wa Uholanzi, Marin wa Romania, Fulkrug wa Ujerumani na Schranz wa Slovakia, kila moja amefunga mara mbili.