Djed Spence aambiwa kachezee Kenya wewe

Muktasari:
- Spence amekuwa mmoja wa wachezaji mahiri Spurs msimu huu baada ya kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kocha Ange Postecoglou.
LONDON, ENGLAND: BEKI wa Tottenham Hotspur, Djed Spence ameambiwa aachane na England na badala yake achague kuichezea Kenya kwenye soka la kimataifa baada ya kocha Thomas Tuchel kumtosa kwenye uteuzi.
Spence amekuwa mmoja wa wachezaji mahiri Spurs msimu huu baada ya kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kocha Ange Postecoglou.
Beki huyo wa pembeni mwanzoni alikuwa akiwekwa benchi na kocha huyo raia wa Australia, lakini baadaye alionyesha kiwango bora kabisa na kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya London.
Hata hivyo, kiwango hicho ambacho kiliwaaminisha wengi angechaguliwa na Tuchel kwenye kikosic hake cha Three Lions kwa ajili ya mechi za Albania na Latvia, imekuwa tofauti, hajachaguliwa.
Jambo hilo halijamkatisha tamaa beki huyo akimwambia beki wa zamani wa Manchester United na England, Rio Ferdinand kwamba bado ana matumaini makubwa ya kuichezea Three Lions kwa siku za baadaye, hivyo atazidisha kupambana ili kupata nafasi kwenye timu hiyo.
Lakini, staa wa zamani wa Kenya, Taiwo Atieno ana mawazo tofauti akimtaka Spence kufikiria kuichezea Harambee Stars kimataifa baada ya sasa kunolewa na aliyekuwa kocha wa Man Utd, Benni McCarthy.
“Nimekuwa nikimfuatilia Djed soka lake kwa miaka minne sasa na ni kwa sababu ni mtu mwenzangu wa London Kaskazini na ana asili ya Kenya. Tofauti na England, hapa kuna vipaji vingi, hasa kwenye eneo la pembeni analocheza, lakini Kenya itampa Djed nafasi ya kuwa mtu mkubwa -si tu uwanjani bali kwenye hatima ya soka la Kenya pia,” alisema.