Ancelotti atinga mahakamani, akana mashataka

Muktasari:
- Ancelotti mwenye umri wa miaka 65, alifikishwa mahakamani Jumatano ya wiki hii ikiwa ni saa kadhaa baada ya timu yake kufuzu fainali ya Copa del Rey.
MADRID, HISPANIA: KOCHA wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, amesisitiza kwamba hana hatia wala wasiwasi katika kesi yake inayomkabili ya udanganyifu na kukwepa kodi.
Ancelotti mwenye umri wa miaka 65, alifikishwa mahakamani Jumatano ya wiki hii ikiwa ni saa kadhaa baada ya timu yake kufuzu fainali ya Copa del Rey.
Licha ya tishio la kifungo cha miaka mitano jela kinachotajwa huenda kikamkuta ikiwa atapatikana na hatia, kocha huyu amesema hana wasiwasi wowote.
Alikanusha pia madai kwamba angejaribu kukubali mashtaka yanayomkabili kwamba ni kweli alikwepa kodi ya Euro 1 milioni ili kupunguziwa adhabu.
Akiwa mahakamani hapo, Ancelotti aliongozana na mwanawe Davide, ambaye alicheza soka lakini sasa anafanya kazi chini ya baba yake katika kikosi cha Real Madrid, pia alikuwepo mkewe Mariann Barrena.
Mawakili wa umma walitangaza mwezi Machi mwaka jana kwamba walikuwa wakitaka kifungo cha miaka minne na miezi tisa kwa kocha huyo wa zamani wa Everton kwa mashitaka mawili ya udanganyifu wa kodi.
Madai yaliyotangazwa hadharani mwezi Machi mwaka jana yalidai kwamba Ancelotti alichukua mapato yake ya haki za picha kupitia mifuko na kampuni za kati kwa lengo la kuepuka kodi.
Mawakili wa umma wanasema bosi huyo wa soka alipata zaidi ya Euro 4 milioni kupitia haki za picha mwaka 2014 na 2015.
Kiasi cha kodi wanachodai alidanganya ni zaidi ya Euro 1 milioni.
Maofisa wa Hazina ya Hispania wameweza kurejesha fedha hizo lakini wanadai Ancelotti alipe mara tatu ya kiasi alichodanganya kama faini.
Lionel Messi alipokea kifungo cha miezi 21 jela kwa udanganyifu wa kodi Julai 2016, baadaye kilibadilishwa kuwa faini ya Euro 252,000.
Cristiano Ronaldo naye aliepuka kifungo cha jela akiwa nchini humo baada ya kukiri kwamba alifanya udanganyifu wa kodi Januari 2019 na badala yake akatozwa faini ya karibia Pauni 16.6 milioni.
Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Xabi Alonso, ambaye anaonekana kuwa huenda akawa kocha wa baadaye wa Real Madrid, alifutiwa kesi ya udanganyifu wa kodi Novemba 2019.
Alikuwa ameonywa kuwa angeweza kwenda jela kwa miaka miwili na nusu kama angepatikana na hatia baada ya mawakili wa umma wa Hispania kupunguza ombi lao la kifungo mwishoni mwa kesi yake mjini Madrid.
Ancelotti aliondoka Everton Juni 2021 kuchukua ajira ya kuwa kocha mkuu wa Real Madrid.
Ijumaa iliyopita kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema: "Sijawahi kuwa na wasiwasi lakini ni wazi inanisikitisha wanaposema kwamba nimeshiriki katika udanganyifu, lakini, tena, nina imani kamili na haki. Natazamia sana kutoa ushahidi Jumatano ijayo."
Real Madrid ilifuzu kwa fainali ya Copa del Rey usiku wa jana kwa ushindi wa mabao 5-4 na itakutana na Barcelona mjini Seville Aprili 26.