Hojlund kutumika dili la Lookman Man Utd

Muktasari:
- Mabosi wa Man United wanatafuta mshambuliaji katika dirisha hili na Ademola ni miongoni mwa walio katika orodha yao licha ya kuonekana wana asilimia kubwa zaidi ya kumsajili Victor Osimhen. Mkataba wa sasa wa Ademola unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu huu amecheza mechi 36 za michuano yote na kufunga mabao 18.
MANCHESTER United inahitaji kumtumia mshambuliaji wao raia wa Denmark, Rasmus Hojlund, mwenye umri wa miaka 22, kama sehemu ya ofa kwenda Atalanta kwa ajili ya kutumika kama sehemu ya mabadilishano ili kuipata saini ya mshambuliaji wa timu hiyo wa timu hiyo na Nigeria, Ademola Lookman, 27.
Mabosi wa Man United wanatafuta mshambuliaji katika dirisha hili na Ademola ni miongoni mwa walio katika orodha yao licha ya kuonekana wana asilimia kubwa zaidi ya kumsajili Victor Osimhen. Mkataba wa sasa wa Ademola unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu huu amecheza mechi 36 za michuano yote na kufunga mabao 18.
Kocha Ruben Amorim ameruhusu staa Hojlund kutolewa kama sehemu ya ofa kwa sababu haridhishwi na kiwango alichoonyesha hadi sasa.
Callum Hudson-Odoi
ROMA, Napoli na timu mbili za Ligi Kuu England ziko katika mazungumzo na wawakilishi wa Nottingham Forest, kwa ajili ya kuipata saini ya winga wa timu hiyo mwenye umri wa miaka 24, Callum Hudson-Odoi, ambaye mkataba wake unamalizika msimu ujao.
Msimu huu amecheza mechi 32 za michuano yote, amefunga mabao matano na kutoa asisti zilizozaa mabao mengine matatu.
Liam Delap
NEWCASTLE ipo tayari kutoa Pauni 30 milioni kwenda Ipswich Town kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa timu ya taifa ya England ya vijana wenye umri chini ya miaka 21, Liam Delap.
Hata hivyo, ili kutoa kiasi hicho cha pesa, Ipswich itatakiwa kusubiri hadi mwisho wa msimu huu kuona kama Ipswich itashuka daraja au laa kwa sababu kipengele hicho kitakuwa hai mara tu baada ya timu yake kushuka.
Cristian Romero
TOTTENHAM Hotspur wameanza mazungumzo na beki wao kisiki wa kimataifa wa Argentina, Cristian Romero, mwenye umri wa miaka 26, ambaye anawindwa na Real Madrid na Atletico Madrid.
Romero ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Spurs, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Alishinda Kombe la Dunia na Argentina.
Albert Sambi Lokonga
MABOSI wa Sevilla, hawana mpango wa kumsainisha mkataba wa kudumu kiungo wa Arsenal na Ubelgiji, Albert Sambi Lokonga, mwenye umri wa miaka 25, ambaye amepata majeraha mara nne akiwa kwa mkopo kwenye kikosi chao kwa msimu huu.
Katika mkataba wa mkopo wa staa huyu kuna kipengele kinachowawezesha kumsainisha mkataba wa kudumu ikiwa watalipa Pauni 10.25 milioni.
Vinicius Jr
WAWAKILISHI wa klabu ya Real Madrid na mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Brazili, Vinicius Jr, wamesisitiza kuwa hadi sasa bado hawajafikia makubaliano na staa huyo kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia kwenye viunga hivyo.
Vinicius ambaye ambaye msimu uliopita aliwania tuzo ya Balon d’Or, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Marcus Rashford
TOTTENHAM Hotspur imeonyesha nia ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Rashford ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo kwa sasa katika kikosi cha Aston Villa anakocheza kwa mkopo, mkataba wake na Man United unaisha 2028.
Destiny Udogie
TOTTENHAM haitaki kusikiliza ofa kutoka timu yoyote inayohitaji saini ya beki wao wa kushoto na timu ya taifa ya Italia, Destiny Udogie, 22, ambaye tangu kuanza kwa mwaka huu vigogo mbalimbali wanahitaji huduma yake ikiwemo Manchester City.
Msimu huu Udogie amecheza mechi 30 za michuano yote. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.