Enzo Fernandez atua katika rada za Atletico Madrid

Muktasari:
- Ripoti zinaeleza Atletico inataka kutoa Pauni 25 milioni pamoja na kiungo wao Pablo Barrios kama sehemu ya ofa ya staa huyo.
ATLETICO Madrid inahitaji saini ya kiungo wa Chelsea na timu ya taifa ya Argentina, Enzo Fernandez katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Ripoti zinaeleza Atletico inataka kutoa Pauni 25 milioni pamoja na kiungo wao Pablo Barrios kama sehemu ya ofa ya staa huyo.
Hata hivyo, ofa hiyo inaonekana kuwa ndogo sana kiasi kuishawishi Chelsea imuuze fundi huyo iliyemnunua kwa zaidi ya Euro 100 milioni.
Inaelezwa, Atletico inamtumia pia, Julian Alvarez kama sehemu ya ushawishi kwa sababu yupo karibu sana na kiungo huyo.
Tangu msimu huu uanze, Enzo ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2032, amecheza mechi 35 za michuano yote na kufunga mabao matano.
Enzo alianza msimu kwa kusuasua pale Chelsea lakini hatimaye alibadili upepo na kucheza kwa kiwango bora hadi akiwa na Argentina.
Jarell Quansah
NEWCASTLE imetuma ofa kwenda Liverpool kwa ajili ya kumsajili beki wa kati wa timu hiyo, Jarell Quansah, 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Staa huyu raia wa England mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2029 na msimu huu amecheza mechi 22 za michuano yote lakini nyingi kati ya hizo ameingia akitokea benchini.
Beki huyu ameanza kuonyesha ubora wake hadi kuitwa katika timu ya taifa England wiki iliyopita.
Wojciech Szczesny
BARCELONA ipo katika hatua za mwisho kufanya mazungumzo na kipa wao wa kimataifa wa Poland, Wojciech Szczesny ambaye inataka kumsainisha mkataba mpya utakaomwezesha kukaa hadi mwaka 2026.
Barca ambayo ilimsajili staa huyu akiwa huru baada ya kustaafu na hivyo kumrejesha uwanjani kucheza soka, imevutiwa na kiwango alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu.
Pedri
MANCHESTER City inamwangalia kiungo wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Pedri kama mmoja wa mastaa ambao wanaweza kusaidia eneo lao la kiungo ikiwa watamsajili katika dirisha lijalo.
Licha ya nia yao hiyo, ripoti zinaeleza Barca haina mpango wa kumuuza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22. Pedri amezidi kuwa mtu hatari anayeubonda ile mbaya pale kati kila siku zinavyokwenda.
Kepa Arrizabalaga
BOURNEMOUTH ipo katika hatua za mwisho kufikia makubaliano ya kumsajili kipa wa Chelsea, Mhispania Kepa Arrizabalaga ambaye kocha Enzo Maresca amemwambia kuwa atafute timu ya kuichezea kwani hayupo katika mipango yake.
Kepa ambaye msimu huu anacheza kwa mkopo Bournemouth kiwango chake kimelikosha sana benchi la ufundi la timu hiyo kiasi cha kutaka kuipata huduma yake mazima.
Jules Kounde
CHELSEA inatarajia kuwasiliana na Barcelona kwa ajili ya kuulizia uwezekano wa kuipata saini ya beki kisiki wa timu hiyo na timu ya taifa ya Ufaransa, Jules Kounde katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kounde ambaye msimu huu amecheza mechi 44 za michuano yote na kufunga mabao matatu, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Hugo Larsson
ENTRACH Frankfurt imeendelea kusisitiza kwamba inahitaji kiasi cha pesa kisichopungua Pauni 50 milioni kutoka kwa timu yoyote inayohitaji saini ya kiungo wao na timu ya taifa ya Sweden, Hugo Larsson, 20, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Timu kibao ikiwamo Manchester City zinahitaji huduma ya staa huyu lakini changamoto kubwa imekuwa ni ada ya uhamisho.
Jeremie Frimpong
MANCHESTER City imeanzisha mazungumzo kwa ajili ya kumsaini beki wa kulia wa Bayer Leverkusen na timu ya taifa ya Uholanzi, Jeremie Frimpong, 24, katika dirisha lijalo.
Mbali ya Man City staa huyu pia anawindwa na Liverpool ambayo inataka kumsajili katika dirisha lijalo. Mkataba wake unaisha 2028.