Jude ni Zidane mtupu!

Muktasari:
- Kiungo huyo alikuwa miongoni mwa waliotikisa nyavu wakati Los Blancos ilipotinga fainali ya Copa del Rey usiku wa Jumanne. Bao la Antonio Rudiger alilofunga kwenye dakika za nyongeza liliifanya timu hiyo kupata ushindi wa jumla wa mabao 5-4 dhidi ya Real Sociedad baada ya sare ya 4-4 uwanjani Santiago Bernabeu.
MADRID, HISPANIA: JUDE Bellingham ameonyesha mavitu ya maana kabisa uwanjani akiiwezesha Real Madrid kuendelea kufukuzia mataji muhimu msimu huu.
Kiungo huyo alikuwa miongoni mwa waliotikisa nyavu wakati Los Blancos ilipotinga fainali ya Copa del Rey usiku wa Jumanne. Bao la Antonio Rudiger alilofunga kwenye dakika za nyongeza liliifanya timu hiyo kupata ushindi wa jumla wa mabao 5-4 dhidi ya Real Sociedad baada ya sare ya 4-4 uwanjani Santiago Bernabeu.
Real Madrid sasa itakipiga na ama Atletico Madrid au Barcelona kwenye mchezo wa fainali utakaopigwa Aprili 26.
Hata hivyo, kiwango cha Bellingham ndicho kilichowaibua wengi na kumfanya aanze kulinganishwa na Zinedine Zidane.

Kiungo huyo Mwingereza alitawala sehemu ya kiungo kwa kupiga pasi matata na kukokota mipira akiwavuka wachezaji wa Real Sociedad kama alivyokuwa akitaka. Bellingham alipiga pasi nne matata kabisa kwenye mechi hiyo, huku akiwa na wastani wa asilimia 85 ya usahihi wa pasi zake zote alizopiga kwenye mechi hiyo.
Alisababisha friikiki saba, akigusa mpira mara 83 na kulenga golini mara tatu katika mchezo huo.
Na bao lake, alilofunga katika dakika 82 lilikuwa na maana kwamba staa huyo mwenye umri wa miaka 21, sasa amehusika kwenye mabao 60 katika mechi 83 alizochezea Real Madrid.
Tangu alipojiunga na Los Blancos akitokea Borussia Dortmund mwaka 2023, Bellingham amefunga mabao 36 na kuasisti 24. Jambo hilo limemfanya alinganishwe sana na gwiji wa klabu hiyo, Zidane, ambaye pia alikuwa akivaa jezi Namba 5 kama ambayo anavaa Bellingham kwa sasa.
Mfaransa, Zidane alifunga mabao 49 katika mechi 227 alizochezea Real Madrid kwenye eneo la kiungo kati ya 2001 na 2005. Katika nyakati zake klabuni hapo, ameshinda mataji sita, ikiwamo La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bellingham alilinganishwa na uchezaji wa mshindi huyo wa Ballon d’Or baada ya kiwango bora dhidi ya Sociedad.
Jambo hilo limekuwa mjadala kwenye mitandao ya kijamii, ambapo shabiki wa kwanza alisema: “Jude Bellinghan, hata Zidane hakuwa mzuri kiasi hiki.”

Mwingine aliongeza: “Jude Bellingham anamkaribia Zinedine Zidane kwenye soka la kizazi hiki. Matata.”
Wakati huo huo, Zidane mwenyewe huko nyuma aliwahi kumwagia sifa Bellingham baada ya kukoshwa na kiwango chake.
Alipozungumza Februari mwaka jana, Zidane, ambaye aliwahi kuwa kocha wa Los Blancos baada ya kustaafu soka kama mchezaji, alisifu ubora wa Mwingereza huyo katika msimu wake wa kwanza Bernabeu.
“Usingeweza kufikiria kile ambacho angekwenda kufanya, lakini amevuka matarajio yote kutokana na takwimu zake,” alisema Zidane na kuongeza. “Ona umri wake, unaweza kusahau kwamba ndiyo kwanza ana miaka 20.”
Bellingham sasa anafukuzia kile ambacho hata Zidane alishindwa kukifikia Real Madrid.
Kikosi hicho cha kocha Carlo Ancelotti bado kina uwezo wa kushinda mataji matatu msimu huu baada ya kutinga fainali ya Copa del Rey final. Huko kwenye La Liga ipo nyuma kwa pointi tatu dhidi ya Barcelona na bado kuna mechi tisa.
Kati ya mechi tisa zilizobaki kumaliza msimu, kimo kipute cha El Clasico kitakachopigwa Barcelona, Mei 11.
Real Madrid imetinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo itakipiga na Arsenal kwenye mechi ya kwanza wiki ijayo. Kocha Ancelotti anafukuzia rekodi bora kabisa baada ya miamba hiyo kushinda mara 15 michuano ya Ulaya.