Kane afunga mjadala rasmi wa kurudi EPL

Muktasari:
- Kane, 31, kwa sasa anahusishwa na mpango wa kurudi Liverpool, lakini mwenyewe amefichua kwamba yupo na furaha kubwa huko anakocheza kwa sasa kwenye kikosi cha miamba ya soka ya Ujerumani, Bayern Munich.
MUNICH, UJERUMANI: STRAIKA, Harry Kane ameamua kuzizima kabisa ripoti za kurudi kwenye Ligi Kuu England mwishoni mwa msimu huu.
Kane, 31, kwa sasa anahusishwa na mpango wa kurudi Liverpool, lakini mwenyewe amefichua kwamba yupo na furaha kubwa huko anakocheza kwa sasa kwenye kikosi cha miamba ya soka ya Ujerumani, Bayern Munich.
Straika huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur aliondoka kwenye Ligi Kuu England, Agosti 2023 miaka kadhaa baada ya kuhusishwa na kuachana na timu hiyo.
Bayern iliilipa Spurs dau la awali la Pauni 82 milioni ili kunasa huduma ya Kane, ambaye amekuwa na kiwango bora kabisa tangu alipotua kwenye Bundesliga.
Licha ya kushindwa kuipa Bayern taji msimu uliopita, ambapo timu hiyo ilikuwa na msimu wa hovyo kwa mara ya kwanza tangu 2011-12, Kane alifunga mabao 44 katika mechi 45 za michuano yote.
Baada ya kusaidia England kufika fainali ya Euro 2024, straika huyo ameendelea kuonyesha kiwango chake bora kwenye kufunga mabao, ambapo hadi sasa msimu huu ameshatikisa nyavu mara 33 katika mechi 38, huku chama lake la Bayern likishikilia usukani wa Bundesliga.
Mkataba wa Kane huko Allianz Arena bado una miaka miwili na nusu hadi Juni 2027 - lakini kumekuwa na uvumi wa kuhusu mkali huyo kurudi kwenye Ligi Kuu England wakati wa dirisha lijalo la majira ya kiangazi litakapofunguliwa.
Iliripotiwa mwezi uliopita kwamba mabingwa watarajiwa wa Ligi Kuu England, Liverpool wameonyesha dhamira ya dhati ya kunasa huduma ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31. Lakini, alipoulizwa kuhusu kurudi England, Kane alisema: “Sina uhakika.”
“Nilishasema hilo muda mrefu, mimi sio mtu wa kufikiria sana mambo ya baadaye. Nina furaha sana hapa. Nadhani tuna timu nzuri sana, kocha mzuri na najiona nipo kwenye wakati mzuri, nataka kucheza kwenye viwango vya juu kwa kadri ninavyoweza.
“Nafahamu mambo mengi yanaweza kubadilika kwenye soka ndani ya muda mfupi tu, lakini kwa sasa akili yangu ipo hapa. Sifikirii ligi nyingine wala timu nyingine. Kwenye soka, napenda kwenda na mdundo na mdundo kwa sasa upo hapa Bayern Munich.”