Enzo Maresca aanza na pigo Man City
Muktasari:
- Maresca, kocha wa zamani wa Chelsea alithibitishwa kuwa mrithi wa Pep Guardiola, akisaini mkataba wa miaka mitatu kuinoa City ambapo ataungana na Willy Caballero pamoja na na Danny Walker katika benchi lake la ufundi.
MANCHESTER, ENGLAND: JANA, siku ambayo alitangazwa kuwa kocha mpya wa Manchester City, Enzo Maresca, alianza kwa kupokea habari mbaya kuhusu kikosi chake ikielezwa kwamba kiungo na mshindi wa Ballon d’Or 2024, Rodrigo Hernandez Cascante maarufu Rodri atakuwa nje kwa muda mrefu akisubiri kufanyiwa upasuaji wakati wowote.
Maresca, kocha wa zamani wa Chelsea alithibitishwa kuwa mrithi wa Pep Guardiola, akisaini mkataba wa miaka mitatu kuinoa City ambapo ataungana na Willy Caballero pamoja na na Danny Walker katika benchi lake la ufundi.
Hata hivyo, kocha huyo wa Italia ataanza msimu bila nyota huyo muhimu katika kikosi hicho anayechukuliwa kuwa ndiye injini ya uchezeshaji timu.
Rodri anatarajiwa kufanyiwa upasuaji kutokana na majeraha ambayo hayajatangazwa mara tu atakaporejea kutoka kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazoendelea huko Amrika Kaskazini.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30, ambaye pia ni nahodha wa Hispania alikuwa mhimili muhimu wa Manchester City waliotwaa mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu England kati ya 2021 na 2024 chini ya Guardiola. Alikosa sehemu kubwa ya msimu wa 2024/25 kutokana na jeraha kubwa la goti, lakini alirejea na kucheza mechi 21 za ligi msimu uliopita ambapo Man City ilimaliza nafasi ya pili nyuma ya Arsenal.
Rodri alijiunga na Man City akitokea Atletico Madrid 2019 na ameshacheza takribani mechi 300 katika klabu hiyo.
Hata hivyo, kiungo huyo amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia Real Madrid katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
Mchezo wa kwanza wa Maresca akiwa kocha wa Man City utakuwa wa ufunguzi wa msimu wa Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal katika Uwanja wa Wembley Agosti 16, kabla ya kuanza kwa ligi dhidi ya Bournemouth. Awali, alifundisha Parma na Leicester City kabla ya kujiunga na Chelsea.