Gvardiol, Rodri waibua hofu Man City
Muktasari:
- Manchester City kwa sasa ipo katika kipindi cha mabadiliko kufuatia kuondoka kwa kocha wa muda mrefu, Pep Guardiola, baada ya miaka 10 ya mafanikio, huku msaidizi wake wa zamani, Enzo Maresca, akitajwa kuwa mrithi wake.
LONDON, ENGLAND: MUSTAKABALI wa nyota wawili wa Manchester City, Josko Gvardiol na Rodri uko shakani baada ya kukataa kuondoa uwezekano wa kuondoka klabuni msimu huu wa joto, wakisema watafanya uamuzi baada ya kumalizika wka fainali za Kombe la Dunia linalotarajiwa kuanza Juni 11 hadi Julai 19, mwaka huu.
Manchester City kwa sasa ipo katika kipindi cha mabadiliko kufuatia kuondoka kwa kocha wa muda mrefu, Pep Guardiola, baada ya miaka 10 ya mafanikio, huku msaidizi wake wa zamani, Enzo Maresca, akitajwa kuwa mrithi wake.
Wakati huohuo, baadhi ya wachezaji waliodumu kwa muda mrefu kama Bernardo Silva na John Stones tayari wameondoka, hali inayoongeza hofu ya kupoteza nyota wengine muhimu.
Akizungumza kuhusu uvumi wa kuondoka, Gvardiol amesema: "Sote tumeona uvumi kutoka kila upande. Nina furaha Manchester City na nina kila kitu ninachohitaji. Kabla ya kuumia nilicheza karibu kila mchezo na karibu kila dakika. Baada ya Kombe la Dunia, tutajua kitakachotokea."
Naye kiungo Rodri, mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or 2024, alitoa kauli inayofanana na hiyo huku akihusishwa na kuhamia Real Madrid.
"Hiyo ni sehemu ya soka. Kwa sasa nimejikita katika kuwa kiongozi wa timu ya taifa. Huo ndio mwelekeo wangu. Naelewa kelele zinazozunguka, lakini sitapoteza muda wangu kuzizungumzia. Tutaona baada ya Kombe la Dunia," amesema.
Gvardiol hajacheza tangu alipovunjika mguu Januari, lakini ameitwa kwenye kikosi cha Croatia kwa ajili ya Kombe la Dunia na anaweza kukutana na England katika mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo, Juni 17, ambapo Croatia itakuwa na nyota wake mkongwe, Luka Modric.
Tangu ajiunge na Manchester City 2023 kwa ada ya Pauni 77 milioni, Gvardiol amekuwa mmoja wa mabeki bora Ligi Kuu England akicheza mara 122 na kufunga mabao 13.
Kwa upande wa Rodri, mara kadhaa amehusishwa kurejea jijini Madrid baada ya kuondoka Atletico Madrid na kujiunga na Man City 2019.
Katika mahojiano na vyombo vya habari vya Hispania mwezi Machi, amesema: "Wachezaji wengi wamepitia njia hiyo. Si mara moja, lakini baada ya muda. Kwangu mimi, siwezi kuzikataa klabu bora zaidi duniani."