Hispania; Kizazi kipya, ndoto mpya ubingwa wanautaka
Muktasari:
- Hispania ambao waliondolewa hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Dunia 2022 kabla ya kutwaa ubingwa wa Euro 2024 kwa kiwango cha juu, wanatajwa kuwa miongoni mwa timu zenye nafasi kubwa ya kutwaa taji la dunia mwaka huu.
MADRID, HISPANIA: KOCHA wa timu ya taifa la Hispania, Luis de la Fuente tayari ametanga kikosi cha wachezaji 26 kitakachoiwakilisha Hispania kwenye Kombe la Dunia 2026 huku nyota chipukizi Lamine Yamal akijumuishwa, lakini bila ya mchezaji yeyote kutoka Real Madrid. Beki Dean Huijsen naye amekosa nafasi sambamba na Dani Carvajal.
Hispania ambao waliondolewa hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Dunia 2022 kabla ya kutwaa ubingwa wa Euro 2024 kwa kiwango cha juu, wanatajwa kuwa miongoni mwa timu zenye nafasi kubwa ya kutwaa taji la dunia mwaka huu.
Timu hiyo itaanza kampeni yake dhidi ya Cape Verde Juni 15 kabla ya kucheza na Saudi Arabia pamoja na Uruguay katika Kundi H.
De la Fuente amesema hana wasiwasi wowote kuhusu hali za majeraha ya Lamine Yamal, Nico Williams na Mikel Merino, akisisitiza kuwa ana uhakika watakuwa tayari kwa mchezo wa ufunguzi utakaopigwa jijini Atlanta.
Katika hafla iliyofanyika Madrid, De la Fuente aliwataja makipa Unai Simón wa Athletic Club, David Raya wa Arsenal na Joan Garcia wa Barcelona kuwa walinda mlango wake watatu huku Alex Remiro wa Real Sociedad akiachwa nje.
Katika safu ya ulinzi wameitwa Marc Cucurella, Alejandro Grimaldo, Pau Cubarsí, Aymeric Laporte, Marc Pubill, Eric García, Marcos Llorente na Pedro Porro.
Safu ya kiungo imeundwa na Pedri, Fabián Ruiz, Martín Zubimendi, Gavi, Rodri, Alex Baena na Mikel Merino.
Washambuliaji walioteuliwa ni Mikel Oyarzabal, Dani Olmo, Nico Williams, Yéremy Pino, Ferran Torres, Borja Iglesias, Víctor Muñoz pamoja na Lamine Yamal.
Mbali na Huijsen na Carvajal ambao hawakuwa hata kwenye orodha ya awali ya wachezaji 55, beki wa Atlético Madrid, Robin Le Normand, pia ameachwa nje. Kiungo wa Barcelona, Fermín Lopez naye hatakuwepo baada ya kupata jeraha la kuvunjika mguu. “Ni jambo gumu,” anasema De la Fuente alipoulizwa kuhusu kuwaacha baadhi ya wachezaji. “Tunafikiria kila hali inayoweza kutokea kwenye mechi dhidi ya wapinzani wetu na sifa zao. Tumechagua hawa 26 kwa sababu tunaamini wamekidhi mahitaji ya timu. Siangalii kama mchezaji anatoka timu gani.”
Kutokuwepo kwa Huijsen kunamaanisha hakuna mchezaji yeyote wa Real Madrid katika kikosi cha Hispania kwa mashindano hayo.
De la Fuente pia aliwataja wachezaji tisa wa ziada watakaosaidia mazoezini, akiwemo Gonzalo García wa Real Madrid na Marc Bernal wa Barcelona.
Hispania itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Iraq Juni 4 katika mji wa A Coruna kabla ya kusafiri kuelekea Amerika kwa mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Peru utakaochezwa Puebla Juni 8.
Kuhusu hali ya majeruhi, De la Fuente anasema taarifa za madaktari zinaonyesha kuwa Yamal, Williams na Merino watakuwa tayari kucheza dhidi ya Cape Verde Juni 15. “Tupo watulivu sana,” anasema. “Kama hakutakuwa na matatizo mengine, karibu kila mchezaji atakuwa tayari kuanzia mchezo wa kwanza. Madaktari na makocha wa viungo wamekuwa wakitembelea klabu zao na kufanya mawasiliano ya karibu. Sina shaka watakuwa tayari kwa mchezo wa kwanza, na kama si hivyo basi watakuwa tayari kwa wa pili.” Kocha huyo pia aliwasifu Carvajal pamoja na nahodha wa zamani Morata, waliokuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Hispania kwenye Euro 2024.
“Wameacha urithi mkubwa wa uongozi usiosahaulika,” anasema. “Lakini kizazi kinachokuja nyuma yao kiko tayari kabisa na kina ubora uleule.”
HII NDIO HISPANIA
Hispania imekuwa mwanachama wa FIFA tangu kuanzishwa kwake mwaka 1904, licha ya Shirikisho la Soka la Hispania kuanzishwa rasmi mwaka 1909. Timu ya kwanza ya taifa ya Hispania iliundwa mwaka 1920 ikiwa na lengo kuu la kupata timu ambayo ingeiwakilisha Hispania katika Olimpiki za mwaka 1920 zilizofanyika Ubelgiji mwaka huo huo.
Hispania ilicheza mechi yake ya kwanza katika mashindano hayo Agosti 28, 1920 dhidi ya Denmark, waliokuwa washindi wa medali ya fedha katika Olimpiki mbili zilizopita. Hispania ilishinda mchezo huo kwa bao 1-0 na baadaye kumaliza mashindano hayo ikiwa na medali ya fedha.
Hispania ilifuzu kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia la 1934 kwa kuifunga Brazil katika mchezo wao wa kwanza kabla ya kupoteza dhidi ya wenyeji Italia katika robo fainali.
VITA VILITIBUA
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Hispania pamoja na Vita Kuu ya Pili ya Dunia vilizuia Hispania kucheza mechi zozote za ushindani kati ya Kombe la Dunia la 1934 na hatua za kufuzu za michuano ya mwaka 1950.
Katika fainali za mwaka 1950 huko Brazil, Hispania iliongoza kundi lake na kufuzu hatua ya mwisho ambapo ilimaliza nafasi ya nne. Hadi mwaka 2010, hiyo ndiyo ilikuwa nafasi bora zaidi ya Hispania katika Kombe la Dunia.
Hispania ilitwaa taji lake la kwanza kubwa la kimataifa ilipoandaa michuano ya 1964 Euro na kuifunga Umoja wa Soviet mabao 2-1 katika fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu. Ushindi huo uliendelea kuwa taji lao pekee kubwa kwa miaka 44.
Hispania ilichaguliwa kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la 1982, ikafika hatua ya pili ya mashindano hayo na miaka minne baadaye ilifika robo fainali kabla ya kutolewa kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Ubelgiji. Katika UEFA Euro 1984, Hispania ilipoteza fainali dhidi ya Ufaransa.
Hispania ilifika robo fainali ya Kombe la Dunia la 1994. Mechi hiyo iligubikwa na utata baada ya beki wa Italia, Mauro Tassotti, kumpiga Luis Enrique kiwiko ndani ya eneo la hatari la Hispania, hali iliyomsababisha Enrique kutokwa damu nyingi puani na mdomoni lakini tukio hilo halikuonekana wala kupewa adhabu na mwamuzi Sándor Puhl. Kama mwamuzi angeamua kuwa ni kosa, Hispania ingepewa penalti.
Katika Kombe la Dunia la 2002, Hispania ilishinda mechi zake zote tatu za hatua ya makundi kabla ya kuiondoa Jamhuri ya Ireland kwa penalti katika hatua ya pili. Kisha walikutana na wenyeji wenza Korea Kusin katika robo fainali na kupoteza kwa penalti baada ya mabao mawili ya Hispania kukataliwa kwa utata kutokana na madai ya makosa yaliyotokea wakati wa muda wa kawaida na nyongeza.
GWARIDE LA KIBINGWA
Baada ya kutwaa Kombe la Dunia la 2010 nchini Afrika Kusini, maelfu ya mashabiki wa Hispania walijitokeza mitaani kusherehekea mafanikio hayo ya kihistoria.
Timu hiyo ilirejea nyumbani kama mabingwa wa dunia kwa mara ya kwanza katika historia yao baada ya kuifunga Uholanzi bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliochezwa katika dimba la Soccer City mjini Johannesburg.
Baada ya kuwasili nchini Hispania, wachezaji pamoja na benchi lote la ufundi walipokelewa kwa shangwe kubwa katika mji wa Madrid.
Mashabiki walijaa barabarani wakiwa wamevalia jezi nyekundu za taifa hilo, wakipeperusha bendera na kuimba nyimbo za ushindi huku wakisubiri kuona kombe lao la kwanza la dunia likipita mbele yao.
Gwaride kubwa la ushindi lilifanyika katika mitaa ya Madrid huku basi maalumu lililokuwa limewabeba wachezaji likipita mbele ya makao makuu ya Jeshi la Anga la Hispania. Wachezaji waliokuwa juu ya basi hilo wakishangilia, kucheza na kuinua Kombe la Dunia mbele ya umati mkubwa wa watu waliokuwa wamefurika kila upande wa jiji hilo.
Nyota mbalimbali wa kikosi hicho akiwemo Andres Iniesta, aliyefunga bao la ushindi kwenye fainali, Xavi, Iker Casillas na Fernando Torres walionekana wakiongoza sherehe hizo huku mashabiki wakiimba majina yao.
Furaha hiyo ilionekana kuwaunganisha wananchi wa Hispania kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Sherehe hizo zilikuwa alama ya mafanikio makubwa zaidi kuwahi kupatikana katika historia ya soka la Hispania. Ushindi wa Kombe la Dunia 2010 uliifanya Hispania kuwa taifa la kwanza la Ulaya kutwaa taji hilo nje ya bara lao.
SAFARI YA MAFANIKIO
Katika michuano ya UEFA Euro 2008, Hispania ilishinda mechi zote za Kundi D huku Italia wakiwa wapinzani wao katika robo fainali ambapo Hispania ilishinda kwa penalti 4-2. Baadaye walikutana tena na Russia katika nusu fainali na kuwafunga mabao 3-0. Katika fainali, Hispania iliifunga Ujerumani bao 1-0 huku Fernando Torres akifunga bao pekee la mchezo huo na hivyo Hispania kutwaa taji lake la kwanza kubwa tangu ubingwa wa Ulaya wa mwaka 1964. Xavi alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo.
Mwaka uliofuata, Hispania ilimaliza nafasi ya tatu katika 2009 Kombe la Mabara na kuvunja rekodi yao ya kutofungwa katika mechi 35 mfululizo iliyokuwa imeanza Novemba 2006 baada ya kupoteza dhidi ya Marekani.
Katika Kombe la Dunia la 2010, Hispania ilifika fainali kwa mara ya kwanza baada ya kuifunga Ujerumani bao 1-0. Katika mchezo wa fainali dhidi ya Uholanzi, Iniesta alifunga bao pekee la mchezo huo katika muda wa nyongeza.
Baadaye walifuzu UEFA Euro 2012 wakiwa vinara wa Kundi I kwa rekodi ya ushindi wa asilimia 100. Wakawa timu ya kwanza kutetea ubingwa wa Ulaya baada ya kuifunga Italia mabao 4-0 katika fainali huku Torres akitwaa Kiatu cha Dhahabu kama mfungaji bora wa mashindano hayo.
Hispania ilifika fainali ya 2013 Kombe la Mabara lakini ikapoteza dhidi ya wenyeji Brazil na mwaka uliofuata ikaondolewa katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia la 2014.
Katika UEFA Euro 2016 na Kombe la Dunia la 2018, Hispania iliondolewa hatua ya 16 bora katika mashindano yote mawili, ikifungwa 2-0 na Italia na 4-3 kwa penalti dhidi ya Russia baada ya sare ya 1-1.
Katika UEFA Euro 2020 iliyochezwa mwaka 2021 kutokana na janga la COVID-19 kusababisha kuchelewa, Hispania ilifanya vizuri kwa kufika nusu fainali ya mashindano makubwa kwa mara ya kwanza tangu 2012 kabla ya kupoteza kwa penalti 4-2 dhidi ya Italia baada ya sare ya bao 1-1.
Mwaka huo huo walifika fainali ya Mataifa ya Ulaya lakini wakapoteza dhidi ya Ufaransa.
Katika Kombe la Dunia la 2022, Hispania ilimaliza ya pili kwenye kundi lao kabla ya kupoteza kwa penalti 3-0 dhidi ya Morocco baada ya sare tasa ya 0-0, ikiwa ni mara yao ya tatu mfululizo kutolewa katika mashindano makubwa kupitia penalti.
WABABE ULAYA
Hispania ilimaliza nafasi ya kwanza katika kundi lao la UEFA Euro 2024 bila kufungwa bao lolote, kisha ikaifunga Georgia mabao 4-1 katika hatua ya 16 bora. Baadaye waliwaondoa wenyeji Ujerumani katika robo fainali kwa ushindi wa mabao 2-1 na kuifunga Ufaransa kwa matokeo hayo hayo katika nusu fainali na hivyo kufuzu fainali yao ya tano ya Euro ambapo walitwaa taji lao la nne la Ulaya kwa rekodi mpya baada ya kuifunga England mabao 2-1.
Hispania ikawa timu ya kwanza kushinda mechi zote saba katika michuano moja ya Ulaya huku ikiweka rekodi mpya ya kufunga mabao 15 katika mashindano hayo.
Hispania iliendeleza mafanikio yake katika Ligi ya Mataifa ya Ulaya 2024–25 ambapo iliiondoa Uholanzi katika robo fainali na baadaye kuifunga Ufaransa katika nusu fainali na hivyo kufuzu fainali yao ya pili mfululizo na ya tatu kwa ujumla, huku baadhi ya wachambuzi wakilinganisha mafanikio hayo na “enzi ya dhahabu” ya zamani ya Hispania. Kwa ushindi wao dhidi ya Ufaransa, Hispania iliongeza rekodi yao ya kutopoteza mechi hadi kufikia michezo 23 mfululizo.