Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyuma ya pazia pamba za mastaa wa soka Ulaya

Muktasari:

  • Sikia hii, wacheza soka Ulaya ni kama wanamitindo wanapokuwa katika mitoko yao, kwani hupiga mapigo makali, huku wengine wakitokelezea simpo tu, lakini kishua zaidi kutokana na mavazi wanayoweka miilini mwao kuwa ya bei mbaya. Elewa neno BEI MBAYA!

LONDON, ENGLAND: UNAISHIJE bila kujua Kylian Mbappe anapiga mapigo gani anapotoka katika mitoko yake ya kawaida? Vinicius Junior je? Vipi kuhusu supastaa kinda wa soka anayeutikisa ulimwengu wa sasa Lamine Yamal? Wanatokaje lakini? Ni mavazi gani wanapenda kuvaa? Ulishawahi kumuona Jules Kounde, yule beki na winga matata wa Real Madrid?

Sikia hii, wacheza soka Ulaya ni kama wanamitindo wanapokuwa katika mitoko yao, kwani hupiga mapigo makali, huku wengine wakitokelezea simpo tu, lakini kishua zaidi kutokana na mavazi wanayoweka miilini mwao kuwa ya bei mbaya. Elewa neno BEI MBAYA!

Katika kikosi cha Real Madrid kwa mfano, mastaa karibu wote wanashindana kwa mavazi ya bei ghali, na inaeleweka kwamba kila mmoja anavuta kitu cha maana dukani, basi usitarajie siku nyingi kupita akijibiwa na mwenzake au wenzake. Kwa Barcelona ambayo kundi kubwa la vijana wenye umri wa kati ya miaka 17 na 22, mambo ni zaidi. Madogo wako vizuri kushindana kwa mavazi sambamba na mitoko.

Achana na wachezaji wa timu hizo mbili kubwa za LaLiga, sasa twende Ufaransa. Huko ndiko unaambiwa ushindani wa mavazi ni mkubwa kutokana na kuwapo kwa kampuni nyingi za mitindo ya nguo.

Inaelezwa kwamba wachezaji wengi hasa wenye asili ya Kifaransa, siyo ndani tu ya nchi hiyo hata wanaokipiga nje wanapenda sana kwenda na mitindo mipya ya mavazi, na ndio wanaoongoza kwa mavazi ya kisasa katika ligi kubwa tano za Ulaya. Fuatilia.

Ukiachana na hilo, mastaa wengi wa soka wa Kiingereza wanapenda mavazi simpo, lakini ya bei mbaya. Fikiria suluari anayovaa Harry Kane isiyotofautiana na ile ya mtu wa kawaida Bongo inaweza kumgharimu nyota huyo wa Bayern Munich kiasi kisichopungua Dola 600 hadi 1,500 (kati ya Sh1.3 milioni na milioni 3.8 hivi).

Kwa wanasoka wengi vijana kwa sasa wanapenda kuvaa mashati mapana na suluari pana (bwanga). Mapigo hayo ndiyo yanayowapeleka puta mastaa huko Ulaya hususan Ufaransa na wenye asili ya nchi hiyo wanaocheza nje. Pia staili ya bwanga inavaliwa na nyota wa ile ligi maarufu ya kikapu Marekani maarufu kama NBA.

Lakini ni wachezaji wa nchi gani hasa hupendeza zaidi kuvaa suluari pana? Soka la kisasa halichezwi tu ndani ya uwanja, bali pia nje ya uwanja hasa kwenye mitindo ya mavazi. Katika miaka ya karibuni, suluari pana (wide-leg trousers au baggy pants) zimekuwa sehemu muhimu ya mtindo wa wachezaji wa soka, na baadhi ya wachezaji kutoka mataifa fulani wamejitokeza zaidi kupendeza wanapovaa aina hii ya mavazi.


MASTAA WA KIFARANSA

Kwa nchi hiyo soka na fasheni ni kama pacha. Wachezaji wa Kifaransa wako juu linapokuja suala la mitindo. Ufaransa, hasa Paris, ni miongoni mwa miji mikubwa ya mitindo duniani, na hilo linaonekana kwa wachezaji wake nyota kama Paul Pogba na Ousmane Dembele.

Nyota hao wamekuwa wakionekana mara kwa mara wamevaa suluari pana zinazokwenda na viatu vya kisasa, makoti ya kifahari au fulana za wabunifu maarufu. Kwao, suluari pana siyo mavazi ya kawaida tu, bali ni mtindo wanaoupenda. Nyota hao na wenzao wanajua kucheza na rangi, vitambaa na miundo, jambo linalowafanya waonekane nadhifu na kuvutia.

WABRAZILI PIA WAMO

Kwa mastaa wa Kibrazili wanapenda zaidi kuiga mitindo kutoka kwa nyota wanaowakuta Ulaya mara baada ya kusajiliwa na timu za huko.

Wachezaji hao wanajulikana kwa soka la uchezaji wa kiufundi na hufurahia boli. Kwa mavazi makali, wengi wao hasa vijana hutua Ulaya wakiwa na mavazi ya kawaida, lakini wakifika huko ni wepesi kujichanganya na kuanza kuvutiwa na nguo kali za wabunifu wa bara hilo.

Lakini, kilicho wazi ni kwamba wanapovaa suluari pana huwa hawalazimishi sana kuonekana wako bomba kama ilivyo kina Mbappé. Wachezaji kama Neymar Jr. na Rodrygo hupendelea suluari pana zilizo huru na mara nyingi zikiwa za mtindo wa mitaani (streetwear). Mchanganyiko wa suluari pana, fulana za kawaida na viatu vya kisasa huwafanya waonekane feshi.


HISPANIA UNADHIFU NA KISASA

Wachezaji wa Spain wamekuwa wakionyesha mtindo unaoelekea zaidi kwenye unadhifu wa kisasa. Ingawa siyo wote wanaopenda suluari pana sana, wale wanaozivaa huzifanya zikae vizuri. Wachezaji vijana kama Pedri na Fermin Lopez wameanza kuonekana wakifuata mtindo wa kisasa wa Ulaya, ambapo suluari pana huvaliwa kwa umakini mkubwa, mara nyingi kwa juu wakiwa na fulana kali au makoti mepesi. Mtindo wao ni wa “clean look” unaovutia bila makeke.


UINGEREZA (STREETWEAR)

England imekuwa kitovu cha mitindo ya mitaani, na wachezaji wake hawako nyuma. Nyota kama Jude Bellingham, Bukayo Saka na Marcus Rashford wameonyesha mapenzi yao kwa suluari pana. Huzivaa katika mitoko yao ya kifahari, lakini wakionekana kawaida sana. Mara nyingi huzivaa sambamba na makoti makubwa au viatu vya kisasa vya gharama kubwa. Mtindo wa mastaa wa Kiingereza unaendana sana na vijana wa kizazi cha sasa.


AFRIKA (UHALISIA NA UTAMBULISHO)

Wachezaji wa Kiafrika pia wameanza kujitokeza katika ulimwengu wa mitindo. Kuanzia Senegal, Ivory Coast, Nigeria hadi Morocco, wachezaji wengi huvaa suluari pana huku wakiongeza mguso wa utamaduni wao. Achraf Hakimi, Victor Osimhen na Wilfried Zaha ni mifano mizuri.

Wanapovaa suluari pana mara nyingi huambatanisha na vito, miwani au mavazi yenye rangi na michoro ya kipekee, jambo linalowafanya waonekane tofauti na wenye mvuto wa asili.

Kwa ujumla, wachezaji wa Kifaransa wanaonekana kuongoza kupendeza zaidi wanapovaa suluari pana, wakifuatiwa kwa karibu na wale wa Brazil na Uingereza.

Hata hivyo, uzuri wa mtindo haupimwi kwa taifa pekee, bali kwa mvaaji anavyojiamini, uelewa wa mitindo na namna mchezaji anavyotupia vazi mwilini mwake. Katika soka la kisasa, mchezaji anaweza kung’ara uwanjani na pia kung’ara nje ya uwanja kwa mtindo wa mavazi aliyopigilia mwilini.