Ivory Coast yatupwa nje Kombe la Dunia, Norway mikononi mwa Brazil
Muktasari:
- Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Dallas mjini Arlington katika jimbo la Texas, Marekani, iliichukua Norway dakika 39 kufunga bao la kwanza kupitia kwa winga Antonio Nusa aliyemalizia pasi nzuri ya nahodha Martin Odegaard.
TEXAS, MAREKANI : WAWAKILISHI wa Afrika katika fainali za Kombe la Dunia 2026, Ivory Coast wameaga michuano hiyo baada ya kufungwa mabao 2-1 na Norway katika mechi ya hatua ya 32 bora.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Dallas mjini Arlington katika jimbo la Texas, Marekani, iliichukua Norway dakika 39 kufunga bao la kwanza kupitia kwa winga Antonio Nusa aliyemalizia pasi nzuri ya nahodha Martin Odegaard.
Norway ilipata bao hilo kutokana na kutumia vyema nafasi iliyopata tofauti na wapinzani wao Ivory Coast ambao hadi dakika 45 za kipindi kwanza walikuwa wameelemewa kwenye umiliki wa mpira, huku wakipiga shuti moja lililolenga lango la washindani wao.
Kipindi cha pili Ivory Coast imejibu mapigo na dakika ya 74 imesawazisha bao kupitia kwa Amad Diallo aliyemalizia pasi ya Nicolas Pepe na kurejesha upya matumaini ya timu hiyo.
Nyota huyo anayeichezea Manchester United ya England amefunga bao hilo akitumia dakika 14, tu uwanjani tangu alipoingia kipindi cha pili dakika ya 60 kuchukua nafasi ya Christ Inao Oulai.
Hata hivyo, ndoto za timu hiyo ya Afrika ya kusonga hatua ya 16, bora ziliingia dosari dakika ya 86 baada ya Erling Haaland kuifungia Norway bao la pili na la ushindi akimalizia pasi ya Patrick Berg.
Ushindi huo unaifanya Norway kufuzu hatua ya 16 bora na itakutana na Brazil iliyoitoa Japan kwa kuifunga mabao 2-1, ambapo mechi kati ya miamba hiyo itapigwa Jumapili, Julai 5, kwenye Uwanja wa New York New Jersey.
Norway ina historia fupi lakini yenye mafanikio ya heshima katika Kombe la Dunia ambapo ilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1938, katika fainali zilizofanyika Ufaransa, kisha kuichukua miaka 56, kushiriki tena Marekani mnamo mwaka 1994.
Katika Michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1998, iliyofanyika Ufaransa, ndio ya mafanikio zaidi baada ya kuifunga Brazil mabao 2-1, Juni 23, 1998 na kufuzu hatua ya 16 bora, ikiwa ni moja ya matokeo bora na ya historia kwa timu hiyo ya Norway.
Baada ya miaka 28, Norway imerejea tena Kombe la Dunia la mwaka 2026, linalofanyika Marekani, Mexico na Canada, ikiwa ni mara ya nne kufuatia 1938, 1994, 1998 na 2026, huku mafanikio makubwa ni kuishia hatua ya 16 bora, mwaka 1938 na 1998.
Kwa upande wa Ivory Coast ni miongoni mwa timu za Afrika zilizosheheni mastaa wakubwa na wenye majina ya kuvutia, ingawa kikosi hicho kimekuwa na wakati mgumu katika michuano ya Kombe la Dunia, huku kikiingia hatua ya mtoano mwaka huu kwa mara yake ya kwanza.
Timu hiyo imerejea Kombe la Dunia la mwaka 2026, baada ya miaka 12, tangu mara ya mwisho iliposhiriki kwenye fainali za mwaka 2014 zilizofanyika Brazil, huku ikiwa ni mara ya nne kwa kikosi hicho kushiriki baada ya 2006, 2010, 2014 na 2026.
Katika ushiriki wa kwanza mwaka 2006, kwenye fainali zilizofanyika Ujerumani, Ivory Coast iliangukia kundi gumu la C na kumaliza nafasi ya tatu na pointi tatu, nyuma ya vinara, Argentina na Uholanzi, huku Serbia and Montenegro ikiwa mkiani.
Kombe la Dunia mwaka 2014, la Brazil, Ivory Coast ilimaliza pia nafasi ya tatu kundi C na pointi tatu, nyuma ya Colombia iliyoongoza na pointi tisa na Ugiriki ikimaliza ya pili na pointi zake nne, huku Japan ikiburuza mkiani na pointi moja.