Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Marcelo Bielsa amtema Suárez Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Suárez ambaye kwa sasa anakipiga Inter Miami, amefunga mabao sita katika mechi 11 za Ligi Kuu ya Marekani (MLS) msimu huu, lakini kiwango hicho hakikutosha kumshawishi Bielsa kumjumuisha kwenye kikosi cha mwisho.

Zikiwa zimebaki siku 10 kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia 2026, kocha wa Uruguay, Marcelo Bielsa amemwacha nje mshambuliaji mkongwe Luis Suárez katika kikosi cha timu hiyo kitakachoshiriki mashindano hayo.

Suárez ambaye kwa sasa anakipiga Inter Miami, amefunga mabao sita katika mechi 11 za Ligi Kuu ya Marekani (MLS) msimu huu, lakini kiwango hicho hakikutosha kumshawishi Bielsa kumjumuisha kwenye kikosi cha mwisho.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 39 alicheza mechi yake ya mwisho akiwa na Uruguay mwaka 2024, huku akibaki mmoja wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa zaidi katika historia ya taifa hilo. 

Suárez ndio mfungaji bora wa muda wote wa Uruguay akiwa amefunga mabao 69 katika mechi 143 za kimataifa alizoichezea nchi yake.

Ni Diego Godín pekee aliyewahi kucheza mechi nyingi zaidi za kimataifa kwa Uruguay akifanya hivyo mara 161 dhidi ya 143 za Suárez.

Wakati Suárez akikosa nafasi, kipa mkongwe Fernando Muslera mwenye mechi 134 za kimataifa amejumuishwa kwenye kikosi hicho, huku beki wa Atlético Madrid, José María Giménez, akiwa katika nafasi ya kufikisha mechi 100 akiwa na timu ya taifa.

Mbali na Suárez, kiungo Nahitan Nández pia ameachwa nje katika kile kinachoelezwa kuwa moja ya maamuzi ya kushangaza zaidi ya Bielsa, licha ya mchango mkubwa alioonyesha kiungo huyo wa Al Qadsia wakati wa mechi za kufuzu Kombe la Dunia.

Habari njema kwa Uruguay ni kurejea kwa kiungo wa Real Madrid, Federico Valverde, ambaye amepona tatizo la majeraha, huku mshambuliaji wa Al Hilal, Darwin Núñez, akitarajiwa kuiongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Katika Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika Marekani, Canada na Mexico, timu ya Taifa ya Uruguay imepangwa Kundi E pamoja na Hispania, Cape Verde na Saudi Arabia.

Kikosi hicho pia kinawajumuisha nyota wengine kama Manuel Ugarte wa Manchester United, Rodrigo Bentancur wa Tottenham pamoja na Ronald Araújo wa Barcelona.

Kuachwa kwa Suárez kunahitimisha uwezekano wa mshambuliaji huyo mkongwe kushiriki Kombe la Dunia kwa mara nyingine, baada ya kuwa sehemu muhimu ya Uruguay katika mashindano hayo kwa zaidi ya muongo mmoja.

 Suárez anakumbukwa zaidi katika tukio la Fainali za Kombe la Dunia 2010 la kuzuia kwa mikono mpira uliokuwa unazama wavuni tukio lililosababisha aonyeshwe kadi nyekundu katika mechi baina ya Ghana na Uruguay.

Hata hivyo, aliyekuwa nahodha wa Ghana, Asamoah Gyan alishindwa kutumia vyema nafasi hiyo mwishoni mwa dakika 120 za ziada baada ya kukosa penalti hiyo iliyogonga nguzo ya juu na kutoka nje.

Katika mtanange huo wa kihistoria ilishuhudiwa Uruguay ikitinga hatua ya nusu fainali baada ya kupata ushindi kwa mikwaju ya penalti 4-2.