Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FIFA yathibitisha Iran kucheza Kombe la Dunia Marekani

Muktasari:

  • Ratiba ya mechi za Iran haitabadilika ambapo mechi zake zitachezwa kama zilivyopangwa huko Los Angeles, Marekani.

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, amesisitiza kuwa timu ya taifa ya Iran itashiriki Kombe la Dunia kama ilivyopangwa, licha ya mvutano wa kivita unaoendelea huko Mashariki ya Kati.

Infantino ametoa kauli hiyo wakati wa mechi ya kirafiki iliyochezwa Uturuki, ambapo Iran iliifunga Costa Rica mabao 5-0.

“Iran watakuwepo Kombe la Dunia. Ndiyo maana tuko hapa. Ni timu imara sana na nina furaha kubwa,” amesema Infantino, katika ziara yake kwenye mchezo huo.

Ameongeza kuwa ratiba ya mechi za Iran haitabadilika na zitachezwa kulingana na upangaji wa makundi ulivyopangwa.

Michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 11, itaandaliwa kwa pamoja na Marekani, Mexico na Canada. Iran imepangwa Kundi G, ambapo itaanza dhidi ya New Zealand Juni 15 jijini Los Angeles, kabla ya kucheza na Ubelgiji Juni 21 kisha kumaliza na Misri Juni 26.

Hata hivyo, ushiriki wa Iran ulikuwa na mashaka kufuatia vita kati ya nchi hiyo na Marekani pamoja na Israel vilivyoanza Februari 28.

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka la Iran (FFIRI), Mehdi Mohammad Nabi, amesema wanaheshimu maamuzi ya FIFA na watafuata kanuni zote zilizowekwa.

“Kinachotuhusu zaidi ni kanuni za FIFA. Tutafuata kila watakachoamua. Nchi mwenyeji pia zina wajibu wa kutimiza makubaliano yao,” amesema Nabi.

Awali, FFIRI ilieleza kuwa ilikuwa kwenye mazungumzo na FIFA kuhusu uwezekano wa kuhamishia mechi za Iran nchini Mexico, endapo hali ya usalama itakuwa tata.

Kwa upande wake, Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, alisema nchi yake iko tayari kuandaa mechi za Iran hatua ya makundi ikiwa kutahitajika.

Katika hatua nyingine, Rais wa Marekani, Donald Trump, awali alidai kuwa Iran itakaribishwa kushiriki, lakini baadaye alitoa kauli tofauti akisema timu hiyo isisafiri kwa sababu za kiusalama.

Iran ilijibu kauli hiyo kwa kusisitiza kuwa hakuna mamlaka yoyote inayoweza kuizuia kushiriki Kombe la Dunia.

Kabla ya mchezo huo wa kirafiki ambao Iran iliichapa Costa Rica mabao 5-0, wachezaji wa Iran walivaa vitambaa vyeusi mkononi na kushika picha za watoto waliodaiwa kuuawa katika mashambulizi ya anga, ikiwa ni ishara ya kuomboleza waathirika wa vita.

Taarifa zinaeleza kuwa shambulio moja lililotokea katika mji wa Minab kusini mwa Iran na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 170, wakiwemo wanafunzi na walimu, baada ya shule ya msingi kushambuliwa kwa kombora linalodaiwa kurushwa kimakosa.

Ripoti ya awali ya uchunguzi wa kijeshi wa Marekani, kama ilivyonukuliwa, inaeleza kuwa kombora la Tomahawk lililenga kimakosa eneo hilo.