Guardiola ataka kuvunja rekodi, apata tena adhabu England
Muktasari:
- Man City iliondoka uwanjani St James’ Park, Jumamosi usiku ikiwa bado kwenye mbio za ubingwa wa Kombe la FA, iliporejea kutoka nyuma baada ya bao la mapema la Harvey Barnes na kushinda 3-1.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola, amesema anataka kuvunja rekodi zote nchini humo baada ya kupata adhabu nyingine ya kufungiwa, huku akisisitiza hataacha kuwatetea wachezaji wake.
Man City iliondoka uwanjani St James’ Park, Jumamosi usiku ikiwa bado kwenye mbio za ubingwa wa Kombe la FA, iliporejea kutoka nyuma baada ya bao la mapema la Harvey Barnes na kushinda 3-1.
Hata hivyo, Guardiola alipata adhabu baada ya kumlalamikia sana mwamuzi wa akiba kipindi cha pili cha mchezo, jambo lililomfanya aonyeshwe kadi ya njano na hivyo kufikisha kadi sita msimu huu.
Kwa mujibu wa kanuni mpya zilizoanza kutumika msimu huu katika Ligi Kuu England, makocha hufungiwa mechi moja wakifikisha kadi tatu za njano, na wakifikisha kadi sita hufungiwa mechi mbili.
Adhabu hiyo itahusu mechi za ligi na Kombe la FA, lakini haitahusu mashindano ya Ulaya au fainali. Hivyo Guardiola ataweza kuwa kwenye benchi la ufundi wakati wa fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Arsenal, Machi 22.
Guardiola alieleza timu pinzani zinaendelea kutumia mbinu zisizo za haki kuwazuia wachezaji wake na anashangaa kwa nini hali hiyo inaendelea kuruhusiwa, aliposema: “Wakati Jeremy Doku anampiga chenga Kieran Trippier na kuelekea peke yake kwenye eneo la hatari, kisha anavutwa kutoka nyuma, siombi kadi ya njano lakini hiyo ni faulo. Nitaitetea timu yangu.”
Guardiola aliongeza kwa mzaha: “Nitawaambia kitu, tuna rekodi zote katika nchi hii, zote. Sasa pia tuna rekodi ya kocha mwenye kadi nyingi za njano. Nataka rekodi zote na sasa nimeipata. Nimefungiwa mechi mbili sasa na nitakwenda mapumzikoni kwa mechi hizo mbili.”