Gundu lamtoa machozi Harry Kane

Muktasari:
- Kamera zilimuonyesha Kane akiwa na machozi baada ya filimbi ya mwisho kwenye Uwanja wa San Siro usiku wa Jumatano, wakati Bayern wakichapika kwa matokeo ya jumla ya mabao 4-3.
MUNICH, ENGLAND: STRAIKA wa Bayern Munich ambaye ni kapteni wa timu ya taifa ya England, Harry Kane, alibubujikwa na machozi baada ya Bayern Munich kutolewa kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Inter Milan ambapo gundu limeendelea kumwandama.
Kamera zilimuonyesha Kane akiwa na machozi baada ya filimbi ya mwisho kwenye Uwanja wa San Siro usiku wa Jumatano, wakati Bayern wakichapika kwa matokeo ya jumla ya mabao 4-3.
Licha ya Kane kufunga bao katika mchezo wa Jumatano na kufanya matokeo yamalizike kwa sare ya mabao 2-2, haikuisaidia Bayern kuepuka kikombe cha kutolewa.
Matokeo haya yameendelea kumuacha Kane, mwenye umri wa miaka 31, bila taji lolote katika maisha yake ya soka licha ya mafanikio yake kwa kuwa mfungaji bora mara kadhaa.
Kane amewahi kuwa karibu sana kushinda mataji makubwa akiwa na klabu na timu ya taifa ambapo alimaliza kama mshindi wa pili katika fainali za Euro mara mbili akiwa na England.
Pia amewahi kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa, Carabao na kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu England, pia akiwa na Bayern walipoteza fainali ya Kombe la Super Cup la Ujerumani.
Nyota wa zamani wa Bayern Munich, Michael Ballack, akizungumza na DAZN, alisema machozi ya Kane yalikuwa ya ishara, kwa kuwa nahodha huyo wa England anajua anakaribia kukosa nafasi ya kushinda mataji makubwa ya soka.
Ballack alisema: “Kila mwaka unapopita bila ya kushinda taji ni jambo la huzuni sana, hata mimi nilikuwa na machozi machoni. Kwa sababu nahisi alikuwa anaweza kufanikisha hilo akiwa na Bayern lakini imeshindikana kwa sasa, kwenye mpira huwa haupati nafasi nyingi.”
Licha ya maumivu ya kutolewa Ligi ya Mabingwa, Kane bado ana matumaini ya kushinda taji lake la kwanza katika maisha yake ya soka katika Bundesliga.
Bayern kwa sasa inaongoza Bundesliga kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya mabingwa watetezi Bayer Leverkusen, huku mechi tano pekee zikiwa zimebakia.
Baada ya kuitoa Bayern, Inter Milan itakutana na Barcelona katika nusu fainali timu waliyoitoa kwenye hatua hiyo hiyo mwaka 2010 kabla ya kuifunga Bayern kwenye fainali na kutwaa taji hilo kwa mara ya mwisho.