Huko Liverpool ni vicheko tu

Muktasari:
- Kwanza Liverpool inahitaji kushinda mechi mbili tu za mwezi huu ili kutawazwa kuwa mabingwa rasmi wa EPL ambapo itaanza wikiendi dhidi ya Leicester ambao ikishinda na Arsenal ikapoteza, rasmi watakuwa mabingwa lakini Arsenal pia ikashinda mechi yao dhidi ya Ipswich, Liverpool itatakiwa kushinda dhidi ya Tottenham ili kuwa bingwa.
LIVERPOOL, ENGLAND: HUENDA ukawa ni mwezi mzuri sana kwa Liverpool kutokana na matukio ambayo yanajiri kwao kuanzia ndani ya uwanja na nje ya uwanja.
Kwanza Liverpool inahitaji kushinda mechi mbili tu za mwezi huu ili kutawazwa kuwa mabingwa rasmi wa EPL ambapo itaanza wikiendi dhidi ya Leicester ambao ikishinda na Arsenal ikapoteza, rasmi watakuwa mabingwa lakini Arsenal pia ikashinda mechi yao dhidi ya Ipswich, Liverpool itatakiwa kushinda dhidi ya Tottenham ili kuwa bingwa.
Mbali ya uwezekano wa kutangaza ubingwa mwezi huu, pia beki wao Trent Alexander-Arnold, ameonyesha maendeleo makubwa katika majeraha yake ya kifundo cha mguu ambapo tayari ameshaanza mazoezi na kikosi cha kwanza.
Beki huyo wa kulia alionekana akifanya mazoezi Jumatano akiwa na kikosi cha kwanza, na yupo katika hatua za mwisho kabla ya kurejea uwanjani.
Alexander-Arnold, mwenye umri wa miaka 26, alishiriki sehemu ya mazoezi pamoja na wachezaji wengine chini ya Arne Slot, lakini hakumaliza programu yote.
Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya England amekuwa nje ya uwanja tangu alipoumia dhidi ya Paris Saint-Germain mwezi uliopita katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa ambapo Liverpool ilitolewa, na tayari amekosa mechi nne hadi sasa.
Wakati Trent anarudi, mashabiki wa Liverpool pia wanasherehekea kusaini mkataba kwa mastaa wao wawili, Mohamed Salah na Virgil van Dijk.
Salah ndio alikuwa mchezaji wa kwanza kusaini mkataba mpya kati ya wale ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu na baada ya yeye, jana Van Dijk pia amesaini.
Van Dijk amesaini mkataba mpya wa miaka miwili ambao utamwezesha kupata Pauni 400,000 kwa wiki.
Hiyo inamaliza tetesi za muda mrefu zilizokuwa zikieleza kwamba yeye, Salah na Trent wanaweza kuondoka mwisho wa msimu.
Hata hivyo, swali pekee ambalo limebaki ni kwa Trent ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu na anahusishwa sana kwenda Real Madrid.
Yote kwa yote, huu ni mwezi wa Liverpool, kula bata na kuinjoi maisha.