Lamine Yamal alivyoirudisha mjini 'Shake Body' ya Skales

Muktasari:
- Yamile aliposti video katika mtandao wa Tiktok aliyojirekodi akiwa na nyota wenzake wa timu ya taifa ya Hispania, Nico Williams na Samuel Omorodion baada ya mchezo kati ya Hispania na Uholanzi wakicheza wimbo huo.
WIKIENDI iliyopita nyota wa Barcelona, Lamine Yamal aliingia kwenye vichwa mbalimbali vya habari za burudani baada ya kufanya chalenji ya wimbo wa 'Shake Body'.
Yamile aliposti video katika mtandao wa Tiktok aliyojirekodi akiwa na nyota wenzake wa timu ya taifa ya Hispania, Nico Williams na Samuel Omorodion baada ya mchezo kati ya Hispania na Uholanzi wakicheza wimbo huo.
Wimbo wa msanii wa Nigeria, Skales uliachiwa miaka 10 iliyopita (mwaka 2024) wakati huo Yamal akiwa na umri wa miaka minane.
Tangu uachiwe miaka hiyo, haukufanya vizuri sana na baada ya chalenji hiyo ni kama wameufufua upya wimbo na umeshasikilizwa na maelfu ya watu duniani katika mitandao mbalimbali.
Mtandao wa Tiktok kwa sasa ndiyo unaoongoza kwa kufanyiwa chalenji na watu kutoka mataifa mbalimbali wakijirekodi na kuposti na kuufanya wimbo huo kurudi upya mjini.

Hii ni kutokana na dansi ya wanasoka hao kuigwa na watu mbalimbali na kuzidi kuupaisha na kwa mujibu wa mtandao wa Sportfy, ndani ya saa 24, ulikuwa umesikilizwa na watu milioni moja, huku Tiktok ukitumiwa na zaidi ya watu milioni 1 waliojirekodi wakicheza dansi hiyo.
Baada ya kupata umaarufu tena juzi, Skales amepanga kuurudia wimbo huo 'remix' ulio na mchanganyiko wa saundi za Afrika Kusini 'Amapiano' kwa lengo la kuendelea kuupa umaarufu kipindi hiki.

USHAWISHI WA YAMAL
Kutokana na kuwa na mashabiki zaidi ya milioni 27 katika mitandao ya Instagram na Tiktok zaidi ya milioni 10, Yamal ameupa kiki wimbo huo kutokana na chalenji hiyo na kwa ambao hawajawahi kuusikia watajua ni mpya.
Kinda huyo mwenye mabao sita na asisti 11 kwa sasa ni mmoja wa mastaa wanaotazamwa zaidi katika La Liga, ligi maarufu duniani na katika ulimwengu wa kidijitali anafuatiliwa kwa mambo mengi ikiwamo video hiyo iliyosambaa haraka.

SKALES MWENYEWE
Majina yake kamili Raoul John Njeng-Njeng. ni mwandishi, mwimbaji na rapa kutoka Nigeria, alizaliwa mwaka 1991 huko Kaduna.
Alianza safari yake ya sanaa mwaka 2000 na wimbo wake wa kwanza 'Kaduna' alioutoa mwaka 2007 ulifanya vizuri na kupokelewa na mashabiki wengi nchini humo.
Wimbo huo ulimfungulia milango ya sanaa kisha akatoa ngoma mbalimbali kama Shaku Shaku ya mwaka 2020, Ajaga na nyinginezo zilizompaisha.
Hadi sasa ana albamu nne, Man of the Year (2015), The Never Say Never Guy (2017), Mr Love (2018) na Sweet Distractions (2022).