Leeds, Burnley zarudi EPL

Muktasari:
- Michezo hiyo miwili ndiyo itakayoamua bingwa wa ligi hiyo namba mbili kwa ukubwa England na kwa sasa Leeds inaongoza ikiwa na pointi 94 sawa na Burnley zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
LEEDS, ENGLAND: Leeds na Burnley zimerejea Ligi Kuu England baada ya kumaliza vinara kwenye msimamo wa Ligi ya Championship England nafasi ya kwanza na ya pili mtawalia huku zikibakisha mechi mbili.
Michezo hiyo miwili ndiyo itakayoamua bingwa wa ligi hiyo namba mbili kwa ukubwa England na kwa sasa Leeds inaongoza ikiwa na pointi 94 sawa na Burnley zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Zote zimecheza mechi sawa (44) na Leeds imefunga mabao 89 huku Burnley ikifunga 61 na inayokamata nafasi ya tatu ni Sheffield yenye pointi 86 na haiwezi kuzifikia za Burnley hata ikipoteza mechi zake mbili zilizobaki.

Leeds ilishuka msimu wa 2022/23 ikimaliza nafasi ya 19 na katika mechi 38 ilivuna pointi 31. Msimu huo, pia ilishuka na Southampton iliyovuna pointi 25 katika mechi 38 na sasa imeshuka kutoka ligi kuu na msimu ujao itacheza Championship sambamba na Leicester City.
Burnley nayo ilishuka msimu wa 2023/24 baada ya kumaliza nafasi ya 19 baada ya kucheza mechi 38 na kuvuna pointi 24, sambamba na Sheffield united iliyoshika mkia na pointi 16 katika mechi 38 na sasa inasubiri kucheza play-off kutafuta nafasi ya timu ya tatu kupanda ligi kuu.

MFUMO WA KUPANDA, KUSHUKA ENGLAND
Mfumo wa kushuka Ligi Kuu England ni timu tatu zilizoshika nafasi za mwisho zinashuka moja kwa moja na kwenda Championship na hadi sasa Southampton na Leicester City tayari zimeshuka, huku Ipswitch Town na West Ham United zikiwa hatarini na zinapambana katika mechi zilizosalia kubaki.
Kwenye kupanda kwenda Ligi Kuu, zinatakiwa kupanda timu tatu kutoka championship, anayeshika nafasi ya kwanza na ya pili zinapanda moja kwa moja huku mshindi wa timu nne kuanzia ya tatu hadi ya sita zinapambana kwa ya tatu na ya nne kukutana, huku ya tano na sita pia zikikutana na washindi baina yao wanakutana Uwanja wa Wembley kusaka timu ya tatu ya kupanda ligi kuu.