Liverpool, Barcelona mguu sawa kwa Jonathan Tah

Muktasari:
- Mabosi wa Barcelona hawana wasiwasi juu ya supastaa huyo kwa sababu mwenyewe ameshaonyesha nia ya kutaka kujiunga nayo mara baada ya mkataba wake kumalizika.
BARCELONA hawana wasiwasi kuhusu mpango wa kutaka kumsajili beki wa Bayer Leverkusen na timu ya taifa ya Ujerumani, Jonathan Tah, mwenye miaka 29, ambaye mkataba wake na vigogo hao wa Bundesliga unatarajiwa kumalizika ifikapo mwishoni mwa msimu huu.
Mabosi wa Barcelona hawana wasiwasi juu ya supastaa huyo kwa sababu mwenyewe ameshaonyesha nia ya kutaka kujiunga nayo mara baada ya mkataba wake kumalizika.
Tah ambaye awali alionekana kuwa na nafasi kubwa ya kutua Bayern Munich, anadaiwa kutaka kujiunga na timu ya nje ya Ujerumani ambapo mbali ya Barca, kumekuwa na ripoti za kuhitajika katika kikosi cha Majogoo wa Anfield, Liverpool ambao wanatarajiwa kuingia sokoni kuongeza nguvu ya mastaa wapya dirisha lijalo.
Hata hivyo, beki huyo ameonyesha nia ya kutaka kuichezea Barcelona akiamini atapata mafanikio makubwa zaidi.
Jesus Rodriguez
REAL Betis wanahitaji Pauni 35 milioni ili kumuuza winga anayekuja juu kwa kasi Mhispania Jesus Rodriguez mwenye umri wa miaka 19, ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2029. Rodriguez ni mmoja kati ya mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Betis na msimu huu amecheza mechi 35 za michuano yote na akafunga mabao manne.
Aaron Ramsdale
WEST Ham United inataka kumsajili kipa wa Southampton na timu ya taifa ya England, Aaron Ramsdale, mwenye miaka 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Ramsdale ambaye ameshuka daraja na Southampton msimu huu mkataba wake unatarajiwa kumalizika ifikapo 2028, ambapo msimu huu chama lake hilo alilojiunga nalo akitokea Arsenal limeshuka daraja, hivyo anaweza kuondoka.
Dominic Calvert-Lewin
NEWCASTLE United wanajiandaa kutoa ofa Burnley ili kuipata saini ya kipa wa timu hiyo, James Trafford, 22, na pia wanakamilisha mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa Everton, Dominic Calvert-Lewin, ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu. Mastaa hao wanatarajiwa kuwa wachezaji wa kwanza kusajiliwa na Newcastle katika dirisha lijalo.
Ademola Lookman
ATALANTA wanahitaji Pauni 51 milioni ili kumuuza mshambuliaji Ademola Lookman, 27, ambaye timu nyingi zinahitaji huduma yake tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Lookman ambaye aliwahi kuichezea Everton, alikuwa na mchango mkubwa msimu uliopita hususan katika michuano ya Europa ambapo Atalanta ilichukua ubingwa.
Mark Flekken
BAYER Leverkusen inamevutiwa na kiwango cha kipa wa Brentford, Mark Flekken, mwenye umri wa miaka 31, na inataka kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Taarifa kutoka Sky Sports zinaeleza, Brentford inahitaji kiasi kisichopungua Euro 15 milioni ili kumuuza staa huyo wa kimataifa wa Uholanzi ambaye mkataba wake katika kikosi hicho unatarajiwa kumalizika 2027.
Frank Onyeka
MABOSI wa Brentford wanataka kumrudisha kiungo wa kimataifa wa Nigeria, Frank Onyeka, mwenye umri wa miaka 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya kuwepo kwa timu kibao zinazotaka kumsajili baada ya kiwango bora alichoonyesha katika kikosi cha Augsburg ambapo anacheza kwa mkopo. Mkataba Brentford unamalizika 2027.
Alex Remiro
MKURUGENZI wa michezo wa Barcelona, Deco, ameanza mazungumzo na wawakilishi wa Real Sociedad ili kuipata saini ya kipa wa timu hiyo na Hispania, Alex Remiro, 30, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Barca inamwangalia kama mbadala wa kipa wake raia wa Ujerumani, Marc-Andre ter Stegen, 32, ambaye amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha ya mara kwa mara.