Spurs kicheko, Man United kilio Europa

Muktasari:
- Ratiba inaonyesha Man United iliyotinga hatua hiyo baada ya ushindi wa jumla wa mabao 7-6 dhidi ya Lyon, itakutana na Bilbao na imekuwa na bahati mbaya inapokutana na timu za Hispania.
MANCHESTER, ENGLAND: MICHUANO ya Europa League inatinga hatua ya nusu fainali na Manchester United, Athletic Bilbao, Bodo/Glimt na Tottenham ndizo zilizotinga kusaka zitakazocheza fainali.
Ratiba inaonyesha Man United iliyotinga hatua hiyo baada ya ushindi wa jumla wa mabao 7-6 dhidi ya Lyon, itakutana na Bilbao na imekuwa na bahati mbaya inapokutana na timu za Hispania.
Hii inakuwa mara ya tatu kwa mashetani hawa wekundu kukutana na Bilbao na imechapwa mbili na sare moja.
Man United pia imekutana katika fainali ya Europa League na Villarreal mwaka 2021 kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 10-11.
Pia ilitolewa na Sevilla hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2017/18, 2019/20 ikapigwa katika nusu fainali na 2022/23 katika robo fainali ya Europa League..
Historia hii huenda ikajirudia tena ingawa itategemea na aina ya mechi ambazo timu zote zitacheza nyumbani na ugenini.
Hali inaonekana kuwa sio mbaya sana kwa Spurs ambayo itakutana na Glimt ya Norway ambayo ndio mara yao ya kwanza kufika hatua hii.
Hakuna historia iliyopo kati ya Spurs na timu hii kwa sababu hazijawahi kukutana ingawa Wanorway hawa wanaonekana kuwa tishio baada ya kuitoa Lazio robo fainali.
Nusu fainali za kwanza zinatarajiwa kupigwa Mei 1 kuanzia saa 4:00 usiku na Man United itaanzia ugenini wakti Spurs ikianzia nyumbani.
Hizi hapa rekodi zilizowekwa baada ya mechi za robo fainali kumalizika.
Spurs ndiyo imeshinda taji hili mara nyingi zaidi (2), lakini wakati huo lilipokuwa likiitwa UEFA Cup kabla halijaitwa UEFA Europa League, Man United imeshinda mara moja wakati Bilbao na Bodo zikiwa hazijawahi kuchukua.
REKODI
Mechi ya Manchester United na Lyon ndiyo ya kwanza katika historia ya mashindano makubwa ya soka barani Ulaya kushuhudia mabao matano (5) yakifungwa baada ya muda wa nyongeza.
Manchester United imekuwa timu ya kwanza katika historia kufunga mabao mawili kwenye dakika ya 120 ya mechi ya Ulaya.
Alhamisi ilikuwa ni mara ya pili katika historia na Manchester United ilishinda kwa mabao 5-4, mara ya kwanza likuwa dhidi ya Arsenal Februari 1958.
Hadi sasa ni wachezaji wawili tu wa England, James Tavernier (mabao 7, pasi 2, msimu wa 2021-22) na Bobby Zamora (mabao 6, pasi 2 , msimu wa 2009-10) ndio wamewahi kuhusika katika mabao mengi katika msimu mmoja wa Europa League kumzidi Dominic Solanke ambaye msimu huu amefunga mabao matatu na kutoa asisti nne.