Waarabu wa Saudia wanamtaka Ancelotti

Muktasari:
- Awali, iliripotiwa Ancelotti angeondoka Madrid mwishoni mwa msimu huu, lakini baada ya kikosi chake kuchapika na vigogo wa Ligi Kuu ya England, Arsenal, katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, sasa inasemekana kocha huyo Muitaliano huenda akaondoka mara baada ya fainali ya Copa del Rey itakayofanyika mwishoni mwa mwezi huu.
MADRID, HISPANIA: MABOSI wa chama cha soka cha Saudi Arabia wanaripotiwa wapo kwenye mazungumzo na wawakilishi wa kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, ambaye huenda akaachana na timu yake mwisho wa msimu huu.
Awali, iliripotiwa Ancelotti angeondoka Madrid mwishoni mwa msimu huu, lakini baada ya kikosi chake kuchapika na vigogo wa Ligi Kuu ya England, Arsenal, katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, sasa inasemekana kocha huyo Muitaliano huenda akaondoka mara baada ya fainali ya Copa del Rey itakayofanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa mujibu wa tovuti ya FootballTransfers, timu ya taifa ya Saudi Arabia tayari imewasiliana na Ancelotti ili achukue nafasi ya kuwa kocha mkuu wa taifa hilo baada ya kuondoka Madrid.
Mwandishi wa habari Duncan Castles amefichua Ancelotti yuko tayari na ameonyesha nia ya kwenda kufanya kazi Saudi Arabia.
Inadaiwa pia rais wa Shirikisho la Soka la Brazil amependekeza jina la Ancelotti ili kuchukua nafasi ya Dorival Junior aliyeondoka, ikiwa ni mipango ya kuifanyia maboresho timu ya taifa hilo iliyo kwenye hali mbaya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Shirikisho la Soka la Saudi Arabia linaandaa mpango wa kuboresha timu yao ya taifa kwa ajili ya Kombe la Dunia la mwaka 2034, ambalo wataandaa na wanamtaka Ancelotti kuwa sehemu ya mchakato huo wa maendeleo.
Kuondoka kwa Muitaliano huyo kutoka Real Madrid baada ya fainali ya Copa del Rey bado hakujathibitishwa rasmi, lakini ikiwa ataondoka basi mechi mbili za La Liga dhidi ya Athletic Club na Getafe zitakuwa mechi zake za mwisho za ligi akiwa kocha wa Real Madrid.