Mke wa Onana alizwa mkoba wa Sh200 milioni

Muktasari:
- Mrembo huyo, mwanamitindo Melanie Kamayou alipokwa vitu vyake hivyo akiwa nje ya mgahawa wa misosi ya Kiitaliano huko Cheshire, Machi 29. Kwenye tukio hilo, mtu mmoja, Liam Ross, 25, anaripotiwa kutiwa nguvuni kutokana na matukio ya uporaji, imeelezwa.
MANCHESTER, ENGLAND: MKE wa kipa namba moja wa Manchester United, Andre Onana ameripotiwa kuporwa na wezi mkoba wake wa Hermes Birkin wenye thamani ya Pauni 62,000 pamoja na saa ya Rolex.
Mrembo huyo, mwanamitindo Melanie Kamayou alipokwa vitu vyake hivyo akiwa nje ya mgahawa wa misosi ya Kiitaliano huko Cheshire, Machi 29. Kwenye tukio hilo, mtu mmoja, Liam Ross, 25, anaripotiwa kutiwa nguvuni kutokana na matukio ya uporaji, imeelezwa.
Wezi hao wamechukua vitu hivyo vya kifahari katikati ya mji huo wa kitajiri, Cheshire. Mrembo Melanie, ambaye amejieleza mtandaoni kama mfamasia, mfanyabiashara na filathropia, mara kadhaa amekuwa akipiga picha akiwa ameweka pozi na vitu vyake hivyo vya thamani na kuviposti mtandaoni.
Moja ya vitu vyake hivyo ni mkoba wa Hermes Birk wenye thamani ya Pauni 62,000, (zaidi ya Sh 215 milioni za Kitanzania) ambao unatajwa ni moja ya mkoba wenye matokeo adimu sana duniani. Mikoba ya Hermes Birkin inauzwa kwa pesa nyingi sana, ambao wa thamani kubwa unaweza kuuzwa kwa bei ya kushangaza, hadi Pauni 1.5 milioni, ambayo ni zaidi ya Sh5.2 bilioni.
Mrembo Melanie amefunga ndoa na kipa huyo wa kimataifa wa Cameroon tangu 2023 na wawili hao wanaripotiwa kuwa na mtoto mmoja wa kiume. Walihamia pamoja England baada ya Onana kusaini kujiunga na Man United akitokea Inter Milan kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi 2023.
Tangu wakati huo amedaka kwenye mechi 92 za Man United, ikiwamo ya kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Nottingham Forest, Jumanne iliyopita. Wanandoa hao kwa sasa wanaishi Alderley Edge, eneo maarufu kabisa kwa makazi ya mastaa wa Ligi Kuu England wa sasa na zamani. Masupastaa kama Cristiano Ronaldo, David Beckham, Rio Ferdinand na Wayne Rooney wanaliita eneo hilo ni nyumbani na sasa wanaoishi kwenye eneo hilo ni Trent Alexander-Arnold, Jordan Henderson, Raheem Sterling na Virgil van Dijk kwa kuwataja kwa uchache, ambapo kwenye maegesho ya magari unayoweza kuyaona huko ni Porsche, Lamborghini na Ferrari tu.