Rio Ferdinand ampa kocha Man United wanne

Muktasari:
- Man United kwa sasa inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England wakiwa na tofauti ya pointi 15 na timu zinazoshika nafasi nne za juu.
MANCHESTER, ENGLAND: LEJENDI wa Manchester United, Rio Ferdinand amewataja wachezaji wanne ambao kocha wa timu hiyo, Ruben Amorim anatakiwa awasajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kuboresha kikosi chake.
Man United kwa sasa inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England wakiwa na tofauti ya pointi 15 na timu zinazoshika nafasi nne za juu.
Kwa sasa nguvu zao wameziwekeza katika michuano ya Europa League na wakibeba kombe watafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya moja kwa moja.
Amorim ameiongoza Man United katika mabadiliko makubwa ya kimfumo tangu achukue ajira kutoka kwa Erik ten Hag, akihama kutoka mfumo wa 4-2-3-1 wa Mholanzi huyo na kuingiza wake wa 3-4-2-1 uliompa mafanikio akiwa na Sporting Lisbon.
Dirisha lililopita la majira ya baridi ambalo ndilo lilikuwa la kwanza kwa Amorim tangu apewe dhamana ya kuiongoza Man United alifanya sajili mbili za Patrick Dorgu aliyejiunga nao akitokea Lecce pamoja na Ayden Heaven alijiunga kutoka Arsenal wote wakiwa ni mabeki ingawa Ayden alisajiliwa kama sehemu ya kikosi cha pili.
Akizungumza katika kipindi chake cha Rio Ferdinand Presents Show, Rio anaamini kuna wachezaji wanne ambao wanaweza kuanza kubadilisha hali Old Trafford na kuiweka Man United kwenye njia nzuri tena.
Mshindi huyo mara sita wa Ligi Kuu England alisema: “Ninakubaliana na Gary Neville wanahitaji wachezaji watano, nadhani wanahitaji wachezaji wanne au watano lakini watazuiwa na masuala ya kanuni za kifedha. Wanahitaji kiungo wa kati wa kucheza pembeni ya Manuel Ugarte, kiungo huyo anapaswa kuwa na uwezo wa kuchukua mpira na kuhamisha kwenda safu ya ushambuliaji hapa wanaweza kumchukua Adam Wharton.”
Kiungo Wharton, 21, kwa sasa yuko Crystal Palace akitokea Blackburn Rovers Januari 2024 na amekuwa na kiwango bora na aliitwa hadi kikosi cha England kilichoshiriki michuano ya Euro mwaka jana.
Kufunga mabao inaonekana tatizo kubwa kwa Man United na Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee wameshindwa kubeba mzigo wa kushambulia.
Hivyo, Ferdinand amesema mshambuliaji ambaye anafurahia msimu mzuri katika Ligi Kuu ya Uturuki, Victor Osimhen anapaswa kusajiliwa ili kuondoa tatizo hilo.
“Tunahitaji uzoefu. Tunahitaji mtu anayejua jinsi ya kufunga. Tunahitaji mtu ambaye anaweza kuja na kuonyesha hawa washambuliaji vijana wa Man United jinsi ya kufanya hivyo. Kama mimi ningekuwa Man United, ningefanya iweze kutokea. Osimhen anaweza kufanya hivyo.”
Ferdinand alimtaja mshambuliaji wa Wolves, Matheus Cunha kama mchezaji wake wa tatu bora ambaye anafikiri anatakiwa kusajiliwa hususani baada ya staa huyo kuweka wazi anataka kuondoka.
“Ameeleza wazi anataka kuondoka hivyo ningeenda kumchukua.”
Jina la mwisho alilotaja Ferdinand lilikuwa ni la mchezaji wa zamani wa akademi ya Manchester City, ambaye ni miongoni mwa mabeki bora wa kulia wanaoongoza Bundesliga, Jeremie Frimpong.