Kisa Vinicius Jr, Madrid yaanza kumnyatia Haaland

Muktasari:
- Madrid inadaiwa kuwaweka katika rada zao mastaa kibao ikiwemo Rafael Leao ikiwa ni sehemu ya kujihami juu ya uwezekano wa kuondoka kwa Vinicius ambaye amepokea ofa nono kutoka kwa matajiri hao wa Saudia.
REAL Madrid inafikiria kutuma ofa kwenda Manchester City kwa ajili ya kuipata saini ya straika wao na timu ya taifa ya Norway, Erling Haaland, 24, dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya kuboresha safu yao ya ushambuliaji ambayo huenda ikampoteza Vinicius Jr anayehusishwa na vigogo wa Saudi Arabia.
Madrid inadaiwa kuwaweka katika rada zao mastaa kibao ikiwemo Rafael Leao ikiwa ni sehemu ya kujihami juu ya uwezekano wa kuondoka kwa Vinicius ambaye amepokea ofa nono kutoka kwa matajiri hao wa Saudia.
Hata hivyo, ili kumpata Haaland, Madrid itatakiwa kuweka mezani ofa kubwa kwani Man City haionekani kuwa tayari kumwachia kwa sasa.
Mkataba wa sasa wa staa huyu wa kimataifa wa Norway unatarajiwa kumalizika mwaka 2034. Msimu huu amecheza mechi 40 za michuano yote na kufunga mabao 30.
Frank Onyeka
MABOSI wa Brentford wanataka kumrudisha kiungo wao wa kimataifa wa Nigeria, Frank Onyeka, mwenye umri wa miaka 27, dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya kuwepo kwa timu mbalimbali zinazohitaji kumsajili baada ya kiwango bora alichoonyesha katika kikosi cha Augsburg na anacheza kwa mkopo. Mkataba wake na Brentford unatarajiwa kumalizika 2027.
Hugo Ekitike
EINTRACHT Frankfurt inahitaji kiasi kisichopungua Euro 100 milioni ili kumuuza straika wao wa kimataifa wa Ufaransa, Hugo Ekitike, 22, ambaye anawindwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu England ikiwa pamoja na Arsenal na Tottenham. Ekitike ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Frankfurt na msimu huu amecheza mechi 42 za michuano yote na kufunga mabao 21.
Yahia Fofana
NEWCASTLE United, Wolverhampton na Brentford zinapambana kuiwania saini ya kipa wa Angers na timu ya taifa ya Ivory Coast, Yahia Fofana, 24, ambaye anauzwa kwa kiasi kisichopungua Pauni 15 milioni. Fofana ni miongoni mwa makipa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Angers, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani.
Jobe Bellingham
CHELSEA inaongoza vita ya kuiwania saini ya kiungo wa kati wa Sunderland na timu ya taifa ya England ya vijana wenye umri chini ya miaka 21, Jobe Bellingham, 19, ambaye pia anahitajika na Manchester United, Arsenal, Tottenham, Brighton na Crystal Palace. Tangu kuanza kwa msimu huu Jobe amecheza mechi 36 za michuano yote na kufunga mabao manne. Mkataba wake unamalizika 2028.
Lorenzo Lucca
MANCHESTER United inaendelea kufanya mazungumzo na mshambuliaji wa Udinese, Lorenzo Lucca, 24, ambaye inataka kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Fundi huyu wa kimataifa wa Italia, amelivutia benchi la ufundi la Man United kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu.
Dejan Kulusevski
TOTTENHAM Hotspur imeanza mazungumzo na wakala wa kiungo wao raia wa Sweden, Dejan Kulusevski, 24, ili kumsainisha mkataba mpya na kumzuia asiondoke dirisha lijalo la majira ya kiangazi na vigogo kibao wameonyesha nia ya kumsajili ikiwamo AC Milan na Napoli. Kocha wa Spurs, Ange Postecoglu bado ana mipango na Dejan na hataki kuona akiondoka. Mkataba wake unamalizika 2028.
Stefan Ortega
BAYER Leverkusen imefikia pazuri katika mazungumzo yao na wawakilishi wa kipa wa Manchester City na timu ya taifa ya Ujerumani, Stefan Ortega, 32, ambaye inaweza kumsajili kwa ada ya uhamisho ya Euro 8 milioni dirisha lijalo. Ortega ni miongoni mwa wachezaji ambao hawapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha Pep Guardiola na mkataba wake unamalizika 2026.