Hakuna rekodi za De Bruyne bila Michele!

Muktasari:
- Akiwa ameshinda mataji sita ya EPL na tuzo mbili za Mchezaji Bora wa msimu, De Bruyne, mzaliwa wa Ubelgiji anashikilia rekodi kama mchezaji wa pili aliyetoa pasi nyingi za mabao EP kwa muda wote nyuma ya Ryan Giggs aliyekipiga Manchester United.
Yule mkali wa pasi za mabao katika Ligi Kuu England (EPL), Kevin De Bruyne hatimaye ataondoka Manchester City mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia timu hiyo kwa mafanikio makubwa ndani ya miaka 10 lakini unajua nini?
Akiwa ameshinda mataji sita ya EPL na tuzo mbili za Mchezaji Bora wa msimu, De Bruyne, mzaliwa wa Ubelgiji anashikilia rekodi kama mchezaji wa pili aliyetoa pasi nyingi za mabao EP kwa muda wote nyuma ya Ryan Giggs aliyekipiga Manchester United.
Katika barua yake fupi ya kutangaza kuondoka Man City aliyoitoa hivi karibuni mtandaoni aliwataja watu wanne, Suri, Rome, Mason na Michele ambaye tunaweza kusema ndio chimbuko la rekodi za kiungo huyo pale EPL.

Mwaka 2014 De Bruyne akiwa anaichezea Wolfsburg FC inayoshiriki Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), alikutana na mrembo mmoja, naye si mwingine bali Michele ambaye alikuja na bahati kubwa katika maisha ya mchezaji huyo.
Tunasema alikuja na bahati maana De Bruyne alishacheza EPL akiwa na Chelsea FC ila mambo hayakumwendea sawa hivyo akatolewa kwa mkopo kwenda Werder Bremen kisha Wolfsburg, nani angetegemea angekuja kuweka rekodi hizo EPL?
Kufikia 2015 ikiwa ni mwaka mmoja wa penzi lake na Michele, De Bruyne anatua katika viunga vya Etihad na kuanzia hapo kila kitu kwake kinabadilika kuanzisha maisha ya soka hadi familia.

"Michele alibadilisha maisha yangu kwa njia nyingi. Niwe muwazi, kusema kweli, sijui ningefanya nini bila yeye," alisema De Bruyne katika mahojiano na mtandao wa The Players' Tribune 2019.
Wawili hao kwa mara ya kwanza walikutana kupitia mtandao wa X, zamani Twitter, huku ndipo walipofahamiana mwaka 2014, jina la De Bruyne halikuwa kubwa kama ilivyo sasa hivyo kila mara aliandika (tweet) kile alichojisikia.
"Nilianza kuweka machapisho Twitter nikiwa na wafuasi elfu chache tu wakati huo, kwa sababu nilikuwa bado kwa mkopo Werder Bremen," alisema wakati akiongea na The Players' Tribune na kuongeza.

"Kwa hiyo niliandika kuhusu mechi au chochote kile, na msichana huyu mrembo alikipenda (like) zaidi. Nilikuwa single wakati huo na rafiki yangu aliona, kwa hiyo akasema, 'anaonekana ni msichana mzuri, unapaswa kumtumia ujumbe'," De Bruyne alikumbushia.
Hata hivyo, De Bruyne hakuwa na moyo wa kuzama DM kwa Michele na kumchapa mistari, sijui mwamba alikuwa domo zege?, hivyo huyo rafiki yake ndiye alituma ujumbe kwa niaba yake, kisha wakakaa wakingojea majibu kutoka kwa bibie.
"Nashukuru, alinisaidia kutuma ujumbe huo, naye Michele akajibu. Tulifahamiana kupitia maandishi kwa miezi michache. Ni rahisi sana kwangu mara tu ninapomjua mtu, kwa hivyo baada ya hapo mambo yalienda vizuri na lilikuwa jambo zuri," alisema De Bruyne.
Akiwa tayari anaichezea Man City, De Bruyne alimvisha Michele pete ya uchumba hapo Desemba 2016 katika mnara wa Eiffel huko Paris, Ufaransa, kisha wakafunga ndoa Juni 26, 2017 huko Sorrento nchini Italia.

Baada ya harusi, Michele aliposti picha zao kwenye Instagram wakibusiana na kuandika, "26.06.2017", huku De Bruyne naye akiposti picha zake na kuandika, "kwa sasa ninajivunia naweza kukuita mke wangu".
Tayari wamejaliwa watoto watatu, kipindi cha uhamisho wake mwaka 2015 kwenda Man City ndipo De Bruyne aligundua mkewe ni mjamzito na katika siku yake ya kuzaliwa akitimiza umri wa miaka 29 alimtaja Michele kama mama bora.
Watoto wao watatu ambao ni Mason (2016), Rome (2018) na Suri (2020) ndio De Bruyne aliwataja katika barua yake ya kuaga Man City na kusema wanashukuru kama familia kwa kuwepo katika klabu hiyo na alama iliyoachwa kwao itabaki milele.

Muda wote Michele amekuwa shabiki mkubwa wa De Bruyne ambaye ndani ya EPL amefunga mabao 70 na kutoa basi za mabao 118, huku akitwaa taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) 2022/23 na lile la Kombe la Dunia (FIFA Club) 2023.
"Sina cha kusema mpenzi," aliandika Michele kwenye Instagram akiwa amemkumbatia De Bruyne wakiwa uwanjani wakisherehekea ubingwa wa watano wa EPL kwa mumewe.
Mwaka 2023 wakihadhimisha miaka sita ya ndoa yao, De Bruyne alitoa neno, "heri ya kumbukizi ya miaka sita ya ndoa yetu kwa mke wangu mrembo na mama bora kwa watoto wetu watatu".

Mbali na kuitunza familia, Michele ni mtangazaji mwenza katika podcast ya Secret Society ambayo inajadili masuala ya kuwainua wanawake, pia yeye na mumewe wanafanya kazi na shirika la hisani la Rays of Sunshine ambalo hutoa misaada kwa watoto.
Desemba 2019 waliwatembelea watoto katika hospitali ya Manchester kama sehemu ya kampeni ya Roc Nation Sports ya Kicks for Kids, Michele alisema ulikuwa wakati mzuri kuona tabasamu kwenye nyuso za watoto hao waliowakaribisha vizuri.