Mlinzi wa Messi apigwa stop!

Muktasari:
- Mlinzi huyo amekuwa akifanya kazi ya kumlinda Muargentina huyo kwenye mechi kwa zaidi ya miaka saba.
MIAMI, MAREKANI: MLINZI wa supastaa Lionel Messi, Yassine Chueko amepigwa marufuku kukaa pembezoni mwa uwanja huko MLS.
Mlinzi huyo amekuwa akifanya kazi ya kumlinda Muargentina huyo kwenye mechi kwa zaidi ya miaka saba.
Messi, 37, alijiunga kwenye ligi ya MLS akichezea kikosi cha Inter Miami katika dirisha la majira ya kiangazi 2023.
Tangu wakati huo amejikuta akivamiwa na mashabiki mbalimbali uwanjani, ambao wengi walikuwa wakitaka kwenda kupiga selfie na supastaa huyo wa zamani wa Barcelona na Paris Saint-Germain.
Chueko amekuwa na kazi ya kumlinda Messi tangu alipokuwa akikipiga Barcelona na Paris Saint-Germain.
Lakini, sasa amepigwa marufuku MLS kukaa pembeni mwa uwanja kutokana na kanuni mpya za ligi.

Chueko alisema: “Hawaniruhusu tena kuingia uwanjani.”
Na mlinzi huyo anaamini MLS inahitaji kufanya kazi kubwa kuwalinda wachezaji, kutokana na Messi peke yake kuvamiwa uwanjani na mashabiki 16 tangu alipojiunga na ligi hiyo.
Cheuko alisema: “Nilikuwa Ulaya kwa miaka saba nikifanya kazi ya kumlinda Messi kwenye Ligue 1 na Ligi ya Mabingwa Ulaya, kuna mashabiki sita tu walivamia uwanjani. Niliwasili Marekani, ndani ya miezi 20 tu, mashabiki 16 tayari wameshavamia uwanjani. Kuna tatizo kubwa hapa. Mimi sio tatizo. Waache nimsaidie Messi.
“Naipenda MLS na CONCACAF, lakini ni lazima tufanye kazi pamoja. Napenda kusaidia. Mimi sio bora kuzidi wengine, lakini nina uzoefu wa kutosha wa kufanya kazi Ulaya. Ni sawa, naelewa uamuzi wao, lakini tunapaswa kuwa bora.”
Chueko aliwahi kujieleza anajiona kama ni sehemu ya familia ya Messi.

Mlinzi huyo amejipatia umaarufu kutokana na staili yake ya kuibuka kusikojulikana kwenda kuwakamata mashabiki waaoingia uwanjani kumsogelea Messi.
Alisema: “Najiona kama sehemu ya familia ya Messi, nafanya kazi kubwa kumlinda. Si tu kimwili, bali kisaikolojia pia, kwa sababu ananiamini sana na ananitegemea kwa mengi, namsikiliza sana. Ni mtu mtulivu.”