Osimhen afunguka mustakabali wake Napoli

Muktasari:
- Osimhen ambaye alijiunga na Galatasaray msimu uliopita kwa mkopo kutoka Napoli, amekuwa na msimu wa kipekee Uturuki akifunga mabao 29 katika mashindano yote ikiwemo 21 kwenye Ligi Kuu Uturuki.
ISTANBUL, UTURUKI: STRAIKA wa Napoli, Victor Osimhen amezungumzia mustakabali wake wakati mkataba wa mkopo wa msimu mmoja Galatasaray ukitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Osimhen ambaye alijiunga na Galatasaray msimu uliopita kwa mkopo kutoka Napoli, amekuwa na msimu wa kipekee Uturuki akifunga mabao 29 katika mashindano yote ikiwemo 21 kwenye Ligi Kuu Uturuki.
Kiwango alichoonyesha mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Nigeria kimezivutia timu kadhaa kubwa Ulaya vikiwemo vigogo wa Ligi Kuu England kama Manchester United, Chelsea na Arsenal. Katikati ya tetesi kuhusu klabu anayohusishwa nayo msimu ujao mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 amesema: “Tutafanya uamuzi hivi karibuni. Itaamuliwa kitakachokuwa bora kwangu. Galatasaray itabaki moyoni mwangu daima. Leo ilikuwa siku isiyosahaulika kutwaa taji letu la 25.”
Wengi walitafsiri maneno hayo kama kuaga kwa Osimhen katika timu hiyo ya Uturuki, lakini makamu wa rais wa Galatasaray, Ibrahim Hatipoglu aliiambia gazeti la AS: “Maneno yake hayamaanishi kuwa anaondoka. Alisema hata kama ataondoka katika dakika za mwisho Galatasaray itabaki moyoni mwake daima. Lakini hakusema kuwa anaondoka. Sisi tunataka abaki.”
Osimhen pia anahusishwa na Barcelona pamoja na Juventus msimu wa joto, ingawa inaripotiwa kuwa amekataa ofa kutoka kwa Juventus kwa sababu anataka kujiunga na klabu ya Ligi Kuu England.