Pogba? Subirini kidogo

Muktasari:
- Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye aliwahi kushinda Kombe la Dunia, hajacheza mechi ya ushindani tangu Septemba 2023 baada ya kufungiwa kwa miezi 18 kucheza soka kutokana na kosa la matumizi ya dawa zinazokatazwa michezoni.
TURIN, ITALIA: STAA wa zamani wa Juventus, Paul Pogba amezungumza kuhusu wapi anaweza kutua katika dirisha lijalo akisisitiza kwamba hadi sasa mambo bado.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye aliwahi kushinda Kombe la Dunia, hajacheza mechi ya ushindani tangu Septemba 2023 baada ya kufungiwa kwa miezi 18 kucheza soka kutokana na kosa la matumizi ya dawa zinazokatazwa michezoni.
Pogba aliruhusiwa kurudi kiwanjani Machi mwaka huu, lakini hajapata timu hadi sasa kwani mkataba wake na Juventus ulivunjwa.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 amehusishwa na timu mbalimbali, wakiwamo waajiri wake wa zamani Manchester United, Marseille na timu kutoka Ligi Kuu ya Marekani na Saudi Arabia.
Kwa sasa fundi huyu ameendelea kufanya mazoezi yake binafsi na hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa kati yake na wawakilishi wa timu yoyote.
Kupitia video aliyoiweka katika ukurasa wake wa Instagram, Pogba alisema: "Hakuna cha kusema kwa sasa, bado nina hamu sana ya kurudi, nimekuwa nikifanya mazoezi peke yangu na bado sijakata tamaa. Ujumbe kwa watu wengine ni kwamba kama hupati unachokitaka kwa sasa, pambana kwani inaweza kuwa kesho au baada ya miaka miwili kile unachotaka kitatokea."
Pogba aliachana na Juventus akiwa anaendelea kutumikia adhabu yake. Amekuwa akitumia muda mwingi nchini Marekani tangu wakati huo, pamoja na mkewe Zulay na watoto wao.
Mara kadhaa alionekana katika mechi za timu ya Lionel Messi, Inter Miami.