Raphinha awekewa mzigo wa maana Saudia

Muktasari:
- Fundi huyu wa kimataifa wa Brazil, pia amepewa ofa ya mshahara wa Pauni 151 milioni ambao atalipwa ndani ya miaka minne.
AL-Hilal imewasilisha ofa ya Pauni 75 milioni kwenda Barcelona kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo ya Catalunya, Raphinha, 28, ambaye inahitaji kumsajili katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu.
Fundi huyu wa kimataifa wa Brazil, pia amepewa ofa ya mshahara wa Pauni 151 milioni ambao atalipwa ndani ya miaka minne.
Mabosi wa Al-Hilal wamevutiwa sana na kiwango cha Raphinha ambacho amekionyesha msimu huu ambapo amecheza mechi 49 za michuano yote, amefunga mabao 30 na kutoa asisti za mabao 25.
Mkataba wa sasa wa Raphinha unaisha 2027 na Barca haijafanya uamuzi ikiwa ipo tayari kumuuza au kumbakisha staa huyo na badala yake inasubiria uamuzi wake kama anataka kuondoka.
Milos Kerkez
LIVERPOOL, Real Madrid, na Manchester City ni miongoni mwa timu zilizoonyesha nia ya kumsajili beki wa kushoto wa Bournemouth na timu ya taifa ya Hungary, Milos Kerkez, 21, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Timu hizi zipo kwenye vita kali kwa sasa lakini Bournemouth imeweka wazi kuwa timu yoyote inayomhitaji itatakiwa kulipa kiasi kisichopungua Pauni 45 milioni.
Matheus Cunha
ARSENAL na Aston Villa zimeingia kwenye vita dhidi ya Manchester United katika dili la kuiwania saini ya mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil, Matheus Cunha, mwenye umri wa miaka 25. Hivi karibuni ripoti zimefichua kwamba Cunha ameshafanya makubaliano ya kujiunga na Man United na sasa timu hiyo inafanya mazungumzo na Wolves kwa ajili ya masuala ya ada ya uhamisho.
James McAtee
NOTTINGHAM Forest na Bayer Leverkusen zimekataa tayari kwa ajili ya kumsajili kiungo wa kati wa Manchester City kutoka England mwenye umri wa miaka 22, James McAtee, ikiwa Man City watafanikiwa kumsajili kiungo mshambuliaji wa Forest na England, Morgan Gibbs-White, 25, au kiungo wa Leverkusen na timu ya taifa ya Ujerumani, Florian Wirtz, 21.
Mohammed Kudus
WINGA wa West Ham na timu ya taifa ya Ghana, Mohammed Kudus, 24, ameendelea kuwa kwenye rada za Al-Nassr ya Saudi Arabia inayohitaji huduma yake kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Kudus ambaye ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha West Ham, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Msimu huu amecheza mechi 30 na kufunga mabao matatu.
Joao Felix
MSHAMBULIAJI wa Chelsea na timu ya taifa ya Ureno mwenye miaka 25, Joao Felix, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo AC Milan, ameanza mazungumzo na timu yake ya zamani, Benfica anayoweza kujiunga nayo katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu. Felix anataka kuendelea kusalia barani Ulaya na kucheza soka la kiushindani licha ya kupokea ofa nono kutoka Saudia.
Martin Zubimendi
ARSENAL bado wana matumaini ya kumsajili kiungo wa Real Sociedad na timu ya taifa ya Hispania, Martin Zubimendi, 26, licha ya fundi huyo wa kimataifa wa Hispania, kuwa katika rada za Real Madrid. Zubimendi ambaye msimu huu amecheza mechi 43 za michuano yote na kufunga mabao mawili mkataba wake wa sasa unaisha mwaka 2027.
Junior Firpo
LEEDS United, ambayo imepanda Ligi Kuu wiki hii, inaweza kumpoteza beki wake kutoka Jamhuri ya Dominika mwenye miaka 28, Junior Firpo, anayehitajika na Real Betis ya Hispania katika dirisha lijalo. Firpo alikuwa sehemu muhimu ya mapigano ya Leeds katika kupanda daraja msimu huu, ambapo alicheza mechi 34 za michuano yote. Mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.