Rashford ni Man United tu

Muktasari:
- Rashford alionyesha kiwango bora katika mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG ambao ulimalizika kwa Villa kushinda mabao 3-2 lakini wakatolewa kwa matokeo ya jumla ya 5-4.
MANCHESTER, ENGLAND: MCHEZAJI wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney amesisitiza kuwa Marcus Rashford bado anahitaji kurudi na kuichezea Manchester United licha ya kuendelea kung'ara akiwa kwa mkopo na Aston Villa.
Rashford alionyesha kiwango bora katika mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG ambao ulimalizika kwa Villa kushinda mabao 3-2 lakini wakatolewa kwa matokeo ya jumla ya 5-4.
Rooney ambaye hadi sasa ndio mfungaji bora wa muda wote wa Manchester United akiwa na mabao 253 katika mechi 559, amesisitiza kwamba Rashford bado moyo wake unatamani kuichezea Man United na jambo hilo halitabadilika hivi karibuni.
"Marcus Rashford anataka kuchezea Manchester United, hiyo nina uhakika asilimia 100, ni kijana wa Manchester pia ni shabiki wa Man United, na katika miaka michache iliyopita mambo yalikuwa magumu kwake, aliondoka kwa sababu alihitaji kucheza na hakuwa anataka kukaa kama mchezaji wa akiba na amethibitisha hilo, najua anataka kuacha alama Man United na ili kufanikisha hilo ilikuwa lazima atoke kidogo."
Rashford alikuwa ameondolewa katika kikosi cha kwanza cha Man United chini ya Ruben Amorim baada ya kocha huyo kuona hajitumi.
Alilazimika kuondoka Januari mwaka huu na tangu atue Villa ametoa asisti sita na kufunga mabao matatu katika mechi 15 za michuano yote.