Real Madrid kwa Ancelotti ni suala la muda

Muktasari:
- Ingawa Madrid bado haijatoka katika michuano hiyo kutokana na kipigo hicho cha mabao matatu, hata hivyo, nafasi ya kufuzu robo fainali ni ndogo.
MADRID, HISPANIA: TAARIFA kutoka tovuti ya Relevo zinadai mabosi wa Real Madrid tayari wameshafanya maamuzi ya kumwondoa Kocha Carlo Ancelotti msimu ujao na tayari wameshampata mrithi wake.
Inaelezwa matokeo ya kichapo cha mabao 3-0 ilichopokea Jumanne, kutoka kwa Arsenal yamechangia mabosi wa Madrid kufanya uamuzi wa kuachana na kocha huyo ingawa bado mambo yanaweza yakabadilika lakini suala la kuondoka linaonekana kuwepo kwa asilimia kubwa.
Ingawa Madrid bado haijatoka katika michuano hiyo kutokana na kipigo hicho cha mabao matatu, hata hivyo, nafasi ya kufuzu robo fainali ni ndogo.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja, kumekuwa na ripoti muda wa Ancelotti na Real Madrid unakaribia kuisha, huku vigogo hao wa Hispania wakihusishwa na makocha wengine, wakati Ancelotti naye akihusishwa na timu ya taifa ya Brazil.
Hata hivyo, ripoti mpya kutoka kwa kituo cha habari cha Relevo, Hispania inadai kuondoka kwa Ancelotti kunakaribia na kipigo dhidi ya Arsenal na kufungwa nyumbani na Valencia, vimechangia kocha huyo kuwa katika kitanzi na kocha Xabi Alonso ndiye anaweza kuchukua nafasi yake.
Pia ripoti kutoka kituo kingine cha habari cha Don Balon imeenda mbali zaidi, ikidai Rais wa Real Madrid, Florentino Perez tayari amefanya uamuzi wa kumtimua Ancelotti mwishoni mwa msimu huu.
Mkutano huo na wakurugenzi wake uliodumu kwa zaidi ya saa mbili na ulimalizika kwa uamuzi wa kuvunja mkataba wa Ancelotti mwaka mmoja kabla ya kuisha na kuwa hakutakuwa na kurudi nyuma hata kama kocha huyo raia wa Italia atashinda Ligi ya Mabingwa Ulaya na La Liga msimu huu.