Ronaldo, Messi Uso kwa uso Buenos Aires

Muktasari:
- Ronaldo, mwenye umri wa miaka 40, na Messi, mwenye umri wa miaka 37, wanatajwa kama wachezaji bora kuwahi kutokea katika kizazi hiki wakiwa na jumla ya tuzo 13 za Ballon d'Or ambazo Ronaldo ana tano huku Messi akiwa na nane.
ARGENTINA: MASTAA Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wanaweza kuwa sehemu ya timu moja kwa mara ya kwanza katika maisha yao ya soka, ripoti zinaeleza.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 40, na Messi, mwenye umri wa miaka 37, wanatajwa kama wachezaji bora kuwahi kutokea katika kizazi hiki wakiwa na jumla ya tuzo 13 za Ballon d'Or ambazo Ronaldo ana tano huku Messi akiwa na nane.
Katika kipindi chao walipokuwa wanacheza soka barani Ulaya, walikuwa wakishindanishwa sana kwa mafanikio na matokeo ya uwanjani ambapo baadhi ya mashabiki wanaamini Messi ni bora na wengine Ronaldo ni bora.
Katika mara zote ambazo wamekutana wakiwa na timu zao, Messi ndio anaongoza kuibuka na ushindi mara nyingi zaidi (16), wakati Ronaldo (11) na mechi tisa zikamalizika kwa sare.
Katika mechi ambazo wote walishiriki, Messi amefunga mara 22 huku Ronaldo akiwa na bao moja pungufu akiwa amefunga mara 21.
Wawili hao walicheza dhidi ya kila mmoja kwa mara ya mwisho Januari 19, 2023, wakati wa mechi kati ya Riyadh All Stars na PSG.
Kama ilivyotarajiwa, Messi alifunga na Ronaldo alifunga mabao mawili katika ushindi wa 5-4 kwa upande PSG.
Mashabiki wengi walidhani hiyo ilikuwa mara ya mwisho kwa wawili hao kukutana, hasa ikizingatiwa kwamba Messi sasa anachezea Inter Miami ya Marekani na Ronaldo yuko Al-Nassr ya Saudi Arabia.
Hata hivyo, huenda wakakutana tena na hata kuwa sehemu ya timu moja kutokana na mpango wa mchezaji mwenzao wa zamani Carlos Tevez ambaye anataka kuandaa mechi maalumu ya kumuaga itakayohusisha wachezaji aliowahi kucheza nao ambao wataunda timu mbili.
Taarifa kutoka ESPN inaeleza, nyota hao wawili wanaweza kushiriki katika mechi ya kuagwa kwa Carlos Tevez huko Buenos Aires, Argentina.
"Ndiyo, nitafanya (mechi ya kuagwa)," Tevez aliiambia tovuti ya OLGA.
"Kwa sasa ninachokifanya ni kuangalia muda na siku, Messi na Ronaldo watakuwapo, nitawatafuta mwenyewe bado namba zao ninazo na naongea nao kupitia WhatsApp."
"Edwin Van der Sar atakuwa timu moja na Gianluigi Buffon timu nyingine. Katika safu ya ulinzi, huenda tukawa na Rio Ferdinand, Nemanja Vidic, Giorgio Chiellini, Leonardo Bonucci, Patrice Evra, kaka yangu, ni lazima awepo. Viungo Andrea Pirlo, Paul Scholes, Roman Riquelme na Rooney pia atakuwapo."
Tevez, aliyestaafu kucheza soka mwaka 2022, aliwahi kucheza na Ronaldo akiwa Manchester United na pia alicheza na Messi kwenye timu ya taifa ya Argentina.