Rooney ataka kocha mpya atajwe haraka
Muktasari:
- Rooney amesema kuchelewa kumteua kocha mpya kunaweza kuigharimu United katika mbio za kusajili wachezaji wakubwa wanaolengwa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu England na michuano ya Ulaya.
MANCHESTER, ENGLAND: NYOTA wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney amewataka mabosi wa timu hiyo kufanya maamuzi ya haraka kuhusu kocha mkuu wa kudumu kabla ya dirisha la usajili wa majira ya kiangazi halijaanza rasmi.
Rooney amesema kuchelewa kumteua kocha mpya kunaweza kuigharimu United katika mbio za kusajili wachezaji wakubwa wanaolengwa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu England na michuano ya Ulaya.
Kwa sasa klabu hiyo ipo chini ya kocha wa muda, Michael Carrick aliyerithi kufuatia kufutwa kazi kwa Ruben Amorim mwezi Januari, 2026.
Carrick ameendelea kupewa nafasi kubwa ya kubaki moja kwa moja kutokana na mafanikio aliyoyapata ndani ya muda mfupi, ikiwemo kuirejesha United kwenye michuano ya Ulaya huku akiongoza timu kushinda mechi 10 kati ya 14 alizosimamia.
Rooney alisema United inahitaji kufanya uwekezaji mkubwa wa wachezaji lakini hilo litakuwa gumu iwapo hakutakuwa na uhakika wa nani atakayekuwa kocha wa kudumu.
“Manchester United wanahitaji kuwekeza kwa wachezaji kipindi cha kiangazi ili waweze kushindana kwenye Ligi ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Wanapaswa kuimarisha kikosi kwa sababu kila mtu anaona kuna mapungufu,” alisema Rooney.
Rooney aliongeza kuwa hali ya sintofahamu kwenye benchi la ufundi inaweza kuwafanya baadhi ya mastaa washindwe kujiunga na klabu hiyo.
“Kama mimi ningekuwa mchezaji ambaye Manchester United wanataka kunisajili, swali la kwanza ningeliuliza ni nani atakuwa kocha? Je, kocha huyo ananihitaji? Hivyo ni muhimu klabu kuwa wazi mapema kuhusu suala hilo,” alisema Rooney.
Rooney anaamini Carrick anatosha kupewa majukumu hayo moja kwa moja kutokana na kile alichofanya ndani ya muda mfupi.
Hata hivyo, viongozi wa United bado hawajafanya uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya Carrick huku taarifa zikieleza wanataka kupitia chaguo mbalimbali kabla ya kutangaza jina la kocha huyo.