Rudiger anukia kupewa kibano

Muktasari:
- Tukio hilo la Rudiger lilitokea dakika za nyongeza wakati mchezo ukielekea mwisho na Kylian Mbappe alikuwa akikokota mpira kwenda lango la Barcelona katika harakati za kujaribu kusawazisha.
MADRID, HISPANIA: BEKI kisiki wa Real Madrid, Antonio Rudiger inadaiwa atakutana na adhabu kubwa kwa kumtupia barafu mwamuzi kwenye mchezo wa fainali ya Copa del Rey dhidi ya Barcelona ambao ulimalizika kwa Madrid kuchapwa mabao 3-2 baada ya dakika 120.
Tukio hilo la Rudiger lilitokea dakika za nyongeza wakati mchezo ukielekea mwisho na Kylian Mbappe alikuwa akikokota mpira kwenda lango la Barcelona katika harakati za kujaribu kusawazisha.
Ubao ulikuwa ukisoma 3-2, lakini wakati anakaribia eneo la boksi mwamuzi Ricardo de Burgos Bengoetxea alipouliza filimbi na kusema Mbape alikuwa ameotea.
Jambo hilo liliwakasirisha sana wachezaji na benchi la ufundi la Madrid na katika kuonyesha hasira zao, Lucas Vazquez na Vinicius Junior ambao walishafanyiwa mabadiliko, walikimbia na kuingia uwanjani na kutupa mikono yao kwa hasira kwa mwamuzi kabla ya Rudiger aliyekuwa benchi kutupa barafu.
Vazquez na Rudiger walipokea kadi nyekundu huku Ferland Mendy na Jesus Vallejo wakijaribu kumtuliza Rudiger aliyekuwa akijaribu kuingia uwanjani ili kumshambulia zaidi mwamuzi.
Baada ya kuonekana akielekezwa kwenye chumba cha kubadilisha nguo, Rudiger alitoka tena baada ya mpira kumalizika na raundi hii alikuwa akitaka kumsogelea mwamuzi De Burgos Bengoetxea na wasaidizi wake, ambao walikuwa wakisubiri katikati ya uwanja.
Lakini Luis Llopis, kocha wa makipa wa Real Madrid, na kipa Andriy Lunin kumzuia Rudiger na kumwambia hilo lilikuwa ni wazo baya.
Bellingham, pia aliondolewa uwanjani kwa kumkosoa mwamuzi alikuwa hachezeshi vizuri na aliwapendelea Barcelona.
Rudiger huenda akapokea adhabu kubwa zaidi kutokana na kitendo chake cha kutaka kurudi uwanjani mara yapili ili kumpiga mwamuzi.
Ingawa haijulikani itakuwa ni adhabu gani lakini ripoti za awali zinadai anaweza kufungiwa zaidi ya mechi 10.