VINICIUS JR: Jeuri ya pesa sababu kuwakataa Waarabu

Muktasari:
- Ofa ya Saudi ilidaiwa huenda ingempa zaidi ya Pauni 1 milioni kwa wiki kiasi ambacho kinaonekana kikubwa sana lakini aliamua kuikataa.
MADRID, HISPANIA: BAADA ya tetesi za muda mrefu kuhusu kwenda Saudi Arabia, hivi karibuni ilitoka taarifa winga wa Real Madrid, Vinicius Jr hana mpango wa kuondoka na tayari ameshafanya makubaliano na timu yake kwa ajili ya kusaini mkataba mpya.
Ofa ya Saudi ilidaiwa huenda ingempa zaidi ya Pauni 1 milioni kwa wiki kiasi ambacho kinaonekana kikubwa sana lakini aliamua kuikataa.
Unaweza kujiuliza jeuri hii ya pesa anaipata wapi? je ana utajiri gani hadi kufikia sasa, twende kazi.

ANAPIGAJE PESA?
Kwanza ni mshahara wake wa Pauni 20.7 milioni kwa msimu. Ndiye anayeshika nafasi ya tatu kwa wanaolipwa pesa nyingi Madrid. Pia ana mikataba mbalimbali ya udhamini na kampuni kubwa ikiwamo Nike inayomlipa takriban Dola 8 milioni kwa mwaka kwa kuvaa viatu vyenye nembo yao, EA Sports, Playstation na Pepsi, huku Red Bull na TCL Mobile zinampa takriban Dola 10 milioni kwa mwaka.
Kwa jumla anapata Dola 60 milioni mwa mwaka kutokana na madili hayo na kuwa na utajiri wa Dola 55 milioni.

MSAADA KWA JAMII
Anataasisi yake ya Instituto Vini Jr na kwa mwaka anawekeza zaidi ya Euro 1.3 milioni zinazotumika kusaidia masomo ya watoto takriban 35000 na ameanzisha kampeni mbalimbali zenye lengo la kukusanya pesa zinazotumika kusaidia watu wasiojiweza na watoto waishio katika mazingira magumu.

NDINGA
Audi Q8 50 TDI quattro-Dola 97,100
Audi e-tron Sportback 55 quattro-Dola 109,103
Lamborghini Urus-Dola 273,880
Range Rover Sport-Dola 182,325
BMW i4 M50-Dola 87,782
Audi A7 Sportback 50 TDI quattro-Dola 88,910

MJENGO
Anamiliki nyumba ya kifahari Moraleja, Madrid aliyoinunua kwa Dola 10.73 milioni iliyo katika eneo la ekari mbili karibu na kiwanja cha mazoezi cha Madrid.
Ndani ya nyumba hiyo kuna vyumba sita vya kulala, chumba cha mazoezi 'gym', sauna, uwanja wa tenisi na uwanja mdogo wa kuchezea soka.

MAISHA NA BATA
Ni mmoja kati ya wachezaji wanaopenda kula bata hususan msimu unapomalizika na anapokuwa Brazil hualika rafiki zake na kuinjoi maisha.
Kwa sasa yupo katika uhusiano na mrembo Maria Julia Mazalli, raia mwenzake wa Brazil na hadi sasa staa huyu hajapata mtoto.