Simulizi ya kusikitisha kisa cha jina la Lamine Yamal

Muktasari:
- Juu ya namba hiyo 19, yameandikwa maneno mawili, Lamine Yamal. Kwa maana ndiyo majina yake anayoitwa na watangazaji wa mechi anapokuwa uwanjani.
KWENYE kikosi cha Barcelona, kuna mchezaji anavaa jezi Namba 19 mgongoni.
Juu ya namba hiyo 19, yameandikwa maneno mawili, Lamine Yamal. Kwa maana ndiyo majina yake anayoitwa na watangazaji wa mechi anapokuwa uwanjani.
Lakini, ushawahi kujiuliza kwanini mchezaji huyo ameamua kuvaa jezi yenye majina yote hayo mawili, Lamine Yamal?
Na pengine usichokijua, majina hayo hayana uhusiano wowote na familia yake.
Kwanini anaitwa Lamine Yamal? Stori ipo hivi.
Kwanza kabisa, Lamine Yamal ni moja ya wanasoka waliobukia kwa kasi kwa miaka ya hivi karibuni, akicheza kwa kiwango bora kabisa kwenye klabu yake ya Barcelona na timu ya taifa ya Hispania.
Alikuwa na msimu bora kabisa Barcelona kwa msimu uliopita, ambao ulikuwa wa kwanza kwake, alipofunga mara saba katika mechi 50. Msimu huu ameendeleza kuwasha moto na kuwa mmoja wa wachezaji tishio kabisa kwenye soka.
Mwaka jana, akiwa na umri wa miaka 17 aliiwezesha timu ya taifa ya Hispania kushinda ubingwa wa Euro 2024 na kuchaguliwa kuwa Kinda Bora wa fainali hizo. Yamal anafanya mambo yote hayo matamu ndani ya uwanja huku jezi yake mgongoni ikiwa imebeba majina yote mawili, Lamine Yamal.
Kwanini? Hii hapa simulizi ya majina hayo kwenye jezi ya kinda huyo wa Barcelona.
Jina lake kamili kinda huyo ni Lamine Yamal Nasraoui Ebana.
Nasraoui ni ubini wa baba yake, wakati Ebana ni ubini wa jina la mama yake, na Lamine Yamal ni muunganiko wa majina mawili. Kwa kifupi tu, Yamal si jina la ubini wake.
Kinachoelezwa ni kwamba wazazi wake Yamal waliamua kumwita jina la 'Lamine' na 'Yamal' kwa heshima ya watu wawili, ambao waliwasaidia wakati walipopitia kipindi kigumu katika maisha yao kabla ya mtoto huyo kuzaliwa.
Majina ya watu hao wawili, mmoja aliitwa Lamine na mwingine Yamal, ambao waliwasaidia familia ya Yamal katika kipindi kigumu cha maisha ikiwamo kuwalipia kodi ya nyumba.
Baba yake Yamal, ambaye jina lake ni Mounir, aliahidi kwamba endapo kama watapata mtoto, basi watamwita mtoto huyo majina ya watu hao wawili kama ishara ya shukrani kwao kwa msaada wa utu waliyowafanyia.
Mama yake Yamal, mrembo Sheila alizaliwa Bata, Equatorial Guinea na baba yake, Mounir anatokea Larache, Morocco. Lakini, mtoto wao wamechagua kuiwakilisha Hispania kwenye soka la kimataifa baada ya kuzaliwa nchini humo na kukulia kwenye akademia ya klabu ya Barcelona.