Spurs, Man United ni 'Do or Die'

Muktasari:
- Manchester United na Tottenham ndio timu pekee mbili kutoka England ambazo zimeingia hatua hii lakini mbali ya kutamani kuchukua kombe, michuano hii kwa timu hizi ni muhimu zaidi kwani ndio njia pekee iliyobakia kwao ili kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
MANCHESTER, ENGLAND: HATUA ya robo fainali ya michuano ya Europa League kwa mechi za mkondo wa pili inatarajiwa kufanyika leo ambapo timu zote nane zitashuka dimbani kwenye viwanja mbalimbali kupambania tiketi ya kwenda nusu fainali.
Manchester United na Tottenham ndio timu pekee mbili kutoka England ambazo zimeingia hatua hii lakini mbali ya kutamani kuchukua kombe, michuano hii kwa timu hizi ni muhimu zaidi kwani ndio njia pekee iliyobakia kwao ili kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Man United na Spurs zimekuwa zikipitia kipindi kigumu kutokana na matokeo mabovu ambayo zimekuwa zikiyapata hali inayoonyesha kuwa ni ngumu kwao kumaliza ndani ya nafasi tano za juu ambazo zingewawezesha kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kwa sasa Spurs ipo nafasi ya 15, ikiwa na tofauti ya pointi 18 dhidi ya timu inayoshikilia nafasi ya tano katika msimamo wa ligi, wakati Man United iko nafasi ya 14 ikiwa na pointi 38, tofauti ya pointi 17 dhidi ya timu inayoshikilia nafasi ya tano katika msimamo ambao ni majirani zao Manchester City.
Kupanda nafasi za juu inaonekana kuwa ngumu kwa timu hizi kutokana na matokeo ambayo imekuwa ikizipata, hivyo nafasi yao kubwa ya kufuzu Uefa inaonekana kuwa kwenye kushinda taji hili la Europa ambapo mshindi anapata nafasi ya moja kwa moja kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Katika mchezo wa mkondo wa kwanza, Tottenham ilipata matokeo mabaya ya sare ya 1-1 dhidi ya Eintrancht Frankfurt ikiwa nyumbani, hivyo kwenye mechi hii ya marudiano leo itatakiwa kushinda bao 1-0 au zaidi ili kupenya.
Kwa upande wa Man United yenyewe iliambuliwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Olympique Lyon ikiwa ugenini, hivyo itatakiwa kushinda japo 1-0 pia katika mchezo wake nyumbani utakaopigwa Old Trafford.
Mbali ya mechi hizi mbili ambazo zote zitapigwa saa 4:00 usiku, Lazio ikiwa nyumbani itakuwa na kazi ya kupindua matokeo dhidi ya Bodo/Glimt ambapo mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Norway ilikubali kichapo cha mabao 2-0.
Athletic Bilbao itakuwa nyumbani pia kuikaribisha Rangers ambayo mechi ya kwanza iliyopigwa Scotland ilimalizika kwa suluhu (0-0).