Teknolojia mpya ya 'offside' Kombe la Dunia usipime
Muktasari:
- FIFA itaanzisha matumizi ya mfumo wa kisasa wa nusu-otomatiki wa kuamua kuotea (semi-automated offside) kwa waamuzi wasaidizi wa video (VAR), ambao unatarajiwa kufanya uamuzi kwa haraka zaidi na kumruhusu mwamuzi msaidizi kuinua bendera mara moja badala ya kusubiri shambulio likamilike.
MIAMI, Marekani: SUALA la waamuzi wasaidizi kuchelewa kuinua kibendera cha kuotea huenda ikawa historia baada ya FIFA kutangaza teknolojia mpya itakayotumika katika Kombe la Dunia 2026.
FIFA itaanzisha matumizi ya mfumo wa kisasa wa nusu-otomatiki wa kuamua kuotea (semi-automated offside) kwa waamuzi wasaidizi wa video (VAR), ambao unatarajiwa kufanya uamuzi kwa haraka zaidi na kumruhusu mwamuzi msaidizi kuinua bendera mara moja badala ya kusubiri shambulio likamilike.
Mfumo huo utatuma tahadhari ya sauti kwa wakati halisi kwa mwamuzi msaidizi endapo mchezaji atakuwa ameotea kwa zaidi ya sentimita 10.
Matoleo ya awali ya teknolojia hiyo yaliyofanyiwa majaribio katika Kombe la Dunia la Klabu la FIFA na Kombe la Mabara la FIFA yalikuwa yanatoa taarifa tu pale mchezaji alipokuwa ameotea kwa zaidi ya sentimita 50.
Hata hivyo, mwamuzi msaidizi ataendelea kuwa na mamlaka ya kuamua wakati gani ainue bendera na kusimamisha mchezo. Anaweza kuamua kuendelea na mchezo ikiwa atahisi kuna hitilafu ya mfumo, ingawa FIFA imesema imeweka mifumo ya ziada ya usalama ili kuzuia makosa.
Teknolojia hiyo bado haitakuwa na uwezo wa kubaini kwa uhakika matukio ya kuotea yaliyo karibu sana. Pia inaweza kukumbana na changamoto pale wachezaji wanapokuwa wameanguka chini au wanapokuwa wengi katika eneo moja kwa karibu.
Aidha, mfumo huo utatumika tu katika matukio ya kuotea yanayotegemea nafasi ya mchezaji na si yale yanayohitaji tafsiri ya mwamuzi, kama vile kuamua kama mchezaji ameathiri mpinzani bila kugusa mpira.
FIFA inaamini mfumo huo utapunguza malalamiko ya mashabiki na wachezaji pamoja na kupunguza hatari ya majeraha yanayotokana na kuendelea kwa mchezo wakati tayari kuna kuotea dhahiri.
Mwezi Mei 2025, mshambuliaji wa Nottingham Forest, Taiwo Awoniyi, aliwekwa katika hali ya usingizi wa kitabibu baada ya kugongana na goli wakati mwamuzi msaidizi alipochelewesha kuinua bendera ya kuotea.
Avatari za 3D zenye akili bandia
FIFA pia imethibitisha kuwa itatengeneza avatari za 3D zinazofanana kabisa na wachezaji kwa kutumia akili bandia (AI) ili kusaidia kufanya uamuzi sahihi zaidi.
Hii itahusisha kutengeneza nakala za kidijitali za wachezaji wote 1,248 watakaounda vikosi vya wachezaji 26 kutoka timu 48 zitakazoshiriki mashindano hayo.
Kila mchezaji ataingia kwenye chumba maalumu kwa ajili ya kuskaniwa mwili wake, mchakato ambao utachukua sekunde moja tu na kufanyika mara moja wakati wa upigaji picha rasmi kabla ya mashindano.
Kutokana na hilo, michoro ya kuotea itakuwa wazi zaidi na sahihi kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Teknolojia mpya ya kubaini mpira kutoka nje na kuzuia mwonekano wa kipa
FIFA pia imeidhinisha matumizi ya teknolojia inayoweza kubaini ikiwa mpira ulitoka nje ya uwanja kabla ya bao kufungwa.
Mwezi Februari, Aston Villa walifutiwa bao dhidi ya Brentford katika tukio lililozua mjadala kutokana na kutokuwa wazi kama mpira ulikuwa umetoka nje.
Mfumo huo utatengeneza picha ya 3D, sawa na teknolojia ya goli kuvuka mstari, ambayo itaonyesha kwa usahihi mahali mpira ulipokuwa.
Chip iliyowekwa ndani ya mpira pia itaonyesha ni mchezaji gani aliyegusa mpira mara ya mwisho, jambo litakalosaidia VAR kuthibitisha kama uamuzi kama kona yalikuwa sahihi.
Zaidi ya hayo, FIFA imepanua matumizi ya teknolojia ya Real-time 3D Recreation ili kurahisisha uamuzi yanayohusiana na mwonekano wa kipa katika matukio ya kuotea.
Kutakuwa na mitazamo miwili ya kidijitali inayopatikana kwa VAR na watazamaji wa televisheni, ambayo itaiga kile anachokiona kila kipa.
Msimu uliopita kulikuwa na matukio kadhaa ya kuotea ambapo kulikuwa na mjadala kuhusu kama mwonekano wa kipa ulikuwa umeathiriwa na mchezaji aliyeotea. Teknolojia hii mpya inatarajiwa kuwapa waamuzi nyenzo ya ziada ya kufanya uamuzi hayo kwa usahihi zaidi.