TOTAL FUTBOL: Ni wikiendi ya shampeni

Muktasari:
- Hata hivyo, keshokutwa huenda majibu ya maswali mengi juu ya nani atanyakua taji hilo yanaweza kujibiwa kutokana na matokeo ambayo yatajiri.
LONDON, ENGLAND: WIKIENDI hii, Ligi Kuu England itakuwa inaingia katika mzunguko wa 33 ambapo kila timu itakuwa imebakisha mechi tano kabla ya kuhitimisha msimu huu.
Hata hivyo, keshokutwa huenda majibu ya maswali mengi juu ya nani atanyakua taji hilo yanaweza kujibiwa kutokana na matokeo ambayo yatajiri.
Shampeni za ubingwa zinaweza kufunguliwa katika Uwanja wa King Power ambako vinara Liverpool watakuwa wanaumana na wenyeji Leicester City.
Liverpool inaweza kutangazwa bingwa katika uwanja huo kutokana na hali ya mambo ilivyo.
Kwa ujumla Majogoo wa Anfield wana pointi 76 walizokusanya katika mechi 32 baada ya kushinda 23, sare saba na kufungwa mbili.
Kwa sasa inahitaji alama sita bila kujali matokeo ya timu nyingine ili kutangaza ubingwa, ingawa alama zinaweza kupungua kutokana na matokeo ambayo Arsenal itapata katika mchezo dhidi ya Ipswich Town.
Ikiwa Washika Mitutu wa London watapoteza mbele ya Ipswich na Liverpool ikashinda dhidi ya Leicester itakuwa imetangazwa rasmi kuwa bingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Mechi ya Arsenal na Ipswich itakayokuwa nyumbani inatarajiwa kupigwa keshokutwa, Jumapili kuanzia saa 10:00 jioni wakati ile ya Liverpool ikipigwa Jumapili hiyohiyo lakini itakuwa saa 12:30 jioni, hivyo wakati Majogoo wanaingia kuumana na Leicester City tayari watakuwa wanajua matokeo ya mechi ya Ipswich Town.
Ikiwa Arsenal itafanikiwa kushinda mechi, Liverpool itatakiwa kusubiri hadi itakapokutana na Tottenham Hotspur wiki ijayo ambapo ikishinda itakuwa bingwa hata kama Arsenal itashinda mechi zote zilizobaki.
Kwa ujumla Arsenal ina pointi 63 na ikipoteza dhidi ya Ipswich itakuwa imejiondoa rasmi katika mbio za ubingwa kwani hata ikishinda mechi zake tano zitakazosalia itafikisha pointi 78 ambazo Liverpool itazivuka kwa kushinda dhidi ya Leicester.
Keshokutwa kutakuwa na mechi tano ambazo pia zitakuwa na mvuto kutokana na umuhimu wa matokeo kwa baadhi ya timu zitakazocheza.
Mchezo wa mapema kati ya Brighton na Brentford kila timu itakuwa inahitaji sana pointi tatu kuanzia kwa Brighton ambayo ikishinda itazidi kusogelea nafasi za juu zitakazoiwezesha kufuzu kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao. Mechi hiyo itaanza kuanzia saa 11:00 jioni.
West Ham United itakuwa nyumbani kuikaribisha Southampton ambayo tayari imeshashuka daraja, lakini mechi hiyo ni muhimu kwa West Ham ambayo ipo katika nafasi za chini kwenye msimamo.
Bingwa mtetezi, Manchester City itakuwa ugenini kuumana na Everton ambayo imekuwa na matokeo mazuri tangu kocha David Moyes alipopewa mikoba ya kuinoa. Crystal Palace itakuwa nyumbani kuikaribisha Bournemouth ambayo inapambana kupanda juu kutoka nafasi ya nane iliyopo kwa sasa lengo likiwa ni kufuzu michuano ya kimataifa.
Mechi ya mwisho kwa keshokutwa itakuwa kati ya Aston Villa na Newcastle United itakayopigwa kuanzia saa 1:30 usiku.
Keshokutwa, Manchester United ikiwa nyumbani itaikaribisha Wolves kuanzia saa 10:00 jioni muda sawa na mechi ya Fulham dhidi ya Chelsea, ilhali Jumatatu kutakuwa na mechi kali kati ya Tottenham na Nottingham Forest itakayopigwa saa 4:00 usiku.