Tumbishie? James anasema yeye ni bora kuliko Zidane, Modric

Muktasari:
- Akikipiga kwenye klabu ya Leon ya huko Mexico kwa sasa, staa huyo wa Colombia alikumbusha kipindi chake alichokuwa kwenye kikosi cha Real Madrid.
MADRID, HISPANIA: WANASEMA hivi, kama husifiwi, jisifu mwenyewe. Ndicho unachoweza kusema baada ya James Rodriguez kudai kwamba yeye ni mchezaji bora kuzidi Zinedine Zidane.
Akikipiga kwenye klabu ya Leon ya huko Mexico kwa sasa, staa huyo wa Colombia alikumbusha kipindi chake alichokuwa kwenye kikosi cha Real Madrid.
Rodriguez alikumbusha namna alivyotua Madrid, aliposema: “Wakati wa Kombe la Dunia (2014) wakala Jorge Mendes aliniambia Real Madrid wananitaka. Alinionya na kunionya, ‘usiondoke kwenye mstari, sawa,’ na hilo lilinipa nguvu zaidi. Baada ya mechi ya Japan, ambayo niliingia na kufunga bao, kisha dhidi ya Uruguay nilifunga mara mbili, akaniambia nahitaji zaidi. Nilikuwa na miaka 22 na hapo nilijisemea, ‘Sasa napaswa kucheza vizuri’, na hapo nilikwenda kushinda Kiatu cha Dhahabu cha Kombe la Dunia.”

Aliongeza: “Manchester City na PSG pia zilinitaka. Walinipa ofa ya pesa nyingi sana na mshahara mkubwa, lakini nilichagua Madrid kwa sababu Florentino (Perez, rais) alinipigia na kuniambia: ‘Pesa au mataji?’ Siku zote nimekuwa shabiki wa Real Madrid, Real Madrid ni Real Madrid.
“Nilipowasili Madrid nilikuwa nawaza: ‘Nitakwenda kuzungumza nini na Ramos, Karim, Modric, Cristiano au Iker?’ Lakini, niliwasili, wote walikuwa watulivu sana. Florentino Pérez alikuwa akinitendea vizuri. Sikuzungumza naye muda mrefu, lakini nina hakika nilikuwa mmoja wa vipenzi vyake.”
Kwenye mahojiano hayo, James aliulizwa kati yake yeye na Zinedine Zidane nani alikuwa mchezaji bora.
Na hapo ndipo staa huyo aliposema: “Zidane alikuwa mzuri, katika ubora wake alishinda Kombe la Dunia, lakini... James.” Sambamba na hilo, James alijitaja kuwa bora mbele ya Luka Modric, Toni Kroos na Xavi Hernandez, aliposema. “Kwenye bora wangu, James ni balaa.”